UNHCR yatafuta dola milioni 40 kusaidia wakimbizi wa Kongo waliokimbia machafuko

Wakati waasi wa M23 wakiendelea kusonga mble katika mkoa wa Kivu Kaskazini na Kusini, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linaomba zaidi ya dola milioni 40 kusaidia watu waliokimbia makazi yao katika mikoa hii mawili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na katika nchi jirani.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) siku ya Ijumaa lilizindua ombi la dharura la dola milioni 40.4 kushughulikia mzozo wa kibinadamu unaoongezeka ambao unatokana na ghasia zinazoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Tangu mwezi wa Februari, zaidi ya Wakongo 40,000, hasa wanawake na watoto, wamewasili Burundi kutafuta ulinzi wa kimataifa,” amesema mwakilishi wa UNHCR.

Kuongezeka kwa mapigano katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kunasababisha wimbi kubwa la wakimbizi nchini Burundi, ambapo zaidi ya watu 9,000 wamevuka mpaka kwa siku moja, wakikimbia hali mbaya ya maisha, amebainisha Brigitte Mukanga-Eno, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Burundi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva.

Tangu mwanzoni mwa mwezi wa Februari, zaidi ya Wakongo 40,000, hasa wanawake na watoto, wamepata hifadhi nchini Burundi kutafuta ulinzi wa kimataifa, Mukanga-Eno alisema.

Alisisitiza kwamba watu wengi wanachukua hatari kubwa, kuvuka Mto Rusizi kwa boti kwa kuhofia usalama wao.

Wengi wa wakimbizi hawa wanatoka katika maeneo ambayo tayari yamekumbwa na migogoro, kama vile Goma, na wengi wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa, aliongeza.

“Wanaowasili ni Wakongo ambao tayari wamehamishwa ndani ya nchi kutokana na migogoro ya hapo awali, sasa wanalazimika kukimbia tena kutokana na mapigano mapya,” alieleza.

Kulingana na Mukanga-Eno, timu za UNHCR zimeona ongezeko la kutisha la idadi ya watoto wasioandamana na wazazi wao na wanaowasili, wengi wao wakiwa wametenganishwa na familia zao wakati wa safari yao ya hatari.

Shirika hilo pia limekaribisha uamuzi wa serikali ya Burundi wa kuwapa moja kwa moja hadhi ya ukimbizi wale wanaokimbia mzozo, na kuwaruhusu kupata ulinzi na usaidizi wa kibinadamu mara moja.

Hata hivyo, mahitaji ya dharura yanasalia, hasa katika suala la makazi, chakula, usafi wa mazingira na huduma ya matibabu, alisisitiza.

“Kuna hitaji la dharura la makazi, chakula na vyoo pamoja na kuhamishwa kwa wakimbizi wapya wanaowasili katika maeneo mengine ili kupunguza msongamano,” alisisitiza, hasa kutokana na visa vya surua kuripotiwa katika mazingira ya msongamano wa watu.

Katika kukabiliana na mzozo huo, UNHCR na mashirika ya ndani yanasambaza vifaa muhimu na milo kwa wakimbizi wapya wanaowasili. Mipango pia inaendelea kuwahamisha watu binafsi hadi katika eneo la wakimbizi la Musenyi, ambalo linaweza kuchukua hadi watu 10,000, huku serikali ikitafuta kuanzisha maeneo ya ziada ili kupunguza msongamano wa watu.

Wito wa UNHCR pia unajumuisha masharti kwa nchi jirani mbali na Burundi, kama vile Uganda, Rwanda, Tanzania na Zambia, huku shirika hilo likitazamia uwezekano wa kuingia kwa wakimbizi 258,000, wanaotafuta hifadhi na wanaorejea.

Ingawa harakati za kuelekea nchi nyingine jirani zimekuwa za wastani zaidi, huku kukiwa na takriban watu 15,000 waliowasili mwezi Januari, hali bado ni tete, Mukanga-Eno alisisitiza. Alionya: “Bila matumizi ya haraka ya fedha, tuna hatari ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kadiri mzozo unavyozidi kuwa mbaya.”