
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limetangaza mradi wa thamani ya dola milioni 8 sawa na Sh21 bilioni kwa ajili ya kuboresha usimamizi wa maji ya ardhini kati ya Tanzania na Kenya.
Mradi huu unalenga kuhifadhi ekari 400 za msitu wa Mlima Kilimanjaro, unaohifadhi vyanzo vya maji muhimu kwa zaidi ya watu milioni mbili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Machi 6, 2025 alipokutana na kiongozi wa Unesco, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ushirikiano wa kimataifa katika usimamizi wa maji kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan lengo namba sita linalohusu upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kwa wote.
Amesema mfano mzuri wa utekelezaji wa mpango huu ni mradi wa maji wa Kilimanjaro, unaohusisha maeneo ya Rombo na Hai.
“Nina furaha kutangaza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Unesco umetoa matokeo chanya, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa maji chini ya ardhi wa kimataifa wenye thamani ya dola za Marekani milioni nane. Hii ni hatua muhimu tunayostahili kushukuru kwa msaada wake wa kimkakati katika kufanikisha mradi huu,” amesema.
Kwa muktadha huu, amesema Serikali ya Tanzania inatarajia kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Unesco katika sekta ya maji, hasa kwa kuzingatia kuwa kuna vyanzo vya maji vya kimataifa 22 ambavyo shirika hilo lina jukumu la kusimamia.
“Ni wakati muafaka sasa kwa Unesco na Tanzania kuanzisha miradi ya pamoja zaidi ya kutafuta rasilimali kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo ya sekta ya maji, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Aweso.
Pia, amesema katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji uliofanyika New York, alizungumza na mkurugenzi mkuu wa Unesco na walijikita katika maeneo ya kimkakati ikiwamo kujenga uwezo wa taasisi katika tathimini, usimamizi wa maendeleo ya rasilimali za maji chini ya ardhi, kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya maji na mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Audrey Azoulay amewashukuru marais wa Tanzania na Kenya kwa juhudi zao za kulinda rasilimali hii muhimu ya dunia.
“Maji ni uhai, wanawake wako mstari wa mbele katika kuhifadhi rasilimali hiyo, na Kilimanjaro si tu alama ya urembo wa asili bali pia ni chanzo muhimu cha maji kwa jamii za Tanzania na Kenya,” amesema Audrey.
Amesema kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Unesco pia imetangaza msafara wa wapanda mlima wa watu 30, wakiwemo vijana wa Kiafrika, Agosti mwaka huu ili kuhamasisha dunia kuhusu kuyeyuka kwa barafu na athari zake kwa jamii za milimani.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema, “Tayari fedha zimetolewa kwa ajili ya kuchukua maji kutoka Ziwa Chala, lakini bado hatujakidhi mahitaji ya maji kwa asilimia 100, hasa kwa matumizi ya kunywa na kilimo,” amesema Mkenda.
Kwa hivyo, amesema wanapoangalia mradi huu, wanaona fursa kubwa ya kuboresha maisha ya watu wa Wilaya ya Rombo, Wilaya ya Hai, na hata kwa majirani wa Kenya. Hii inawapa sababu zaidi za kushukuru kwa juhudi hizi.
Amesema mafanikio ya ziara ya mkurugenzi huyo yanafungua njia kwa mafanikio makubwa zaidi si tu kwa Tanzania, bali pia kwa Kilimanjaro na mataifa jirani kama Kenya.
Naye Waziri wa Maji na Umwagiliaji Kenya, Eric Mugaa amesema dhamira ya wizara yetu ni kuhakikisha kila Mkenya anapata maji safi, salama na kwa bei nafuu kwa kiwango cha kutosha.
Hata hivyo, amesema changamoto kama mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa miji kwa kasi na ushindani wa matumizi ya maji zinahitaji suluhisho za kibunifu na za pamoja.
“Serikali ya Kenya imejizatiti kuhakikisha upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba sita na matakwa ya kikatiba kuhusu maji na usafi wa mazingira,” amesema Mugaa.
Kama sehemu ya juhudi hizi, tumefanikisha ramani ya maji chini ya ardhi katika kaunti za Tana River, Wajir, na Marsabit, huku juhudi zikiendelea katika Kaunti ya Mandera.