
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation wamezindua mwongozo rahisi kwa wajasiriamali wachanga, wadogo na wa kati (MSMEs), ukiwalenga kuongeza ushiriki wao katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Mpango huo unalenga kuwawezesha MSMEs kwa kuwapatia nyenzo muhimu na maarifa yatakayowasaidia kupanua biashara zao katika masoko ya Afrika.
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Machi 3 2025, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kagahe amesisitiza dhamira ya Serikali katika kuimarisha ukuaji wa MSMEs akibainisha kuwa MSMEs ni nguzo muhimu ya ajira, uvumbuzi na ukuaji jumuishi, hivyo zinachangia pakubwa katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati.
“Serikali inatambua manufaa ya makubaliano haya, ndiyo maana Bunge letu liliridhia mkataba huu mnamo Septemba 2021, hatua iliyoiwezesha nchi yetu kunufaika na soko huru la Afrika. Uamuzi huu unalenga kufungua fursa kwa wajasiriamali wetu kuvuka mipaka ya taifa letu,” amesema Kagahe.
“Ili kunufaika kikamilifu na fursa hizi, wananchi wetu wanapaswa kuwa na taarifa sahihi, maarifa yanayohitajika, na ujasiri wa kuvuka mipaka kutafuta fursa ndani ya mataifa 55 ya bara letu la Afrika. Kile kinachofanyika katika semina ya leo ni sehemu ya mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali wetu kushindana na wenzao katika soko la AfCFTA.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara amesema: “AfCFTA, kama eneo kubwa zaidi la biashara barani Afrika, linatoa fursa kubwa za kuongeza biashara ya ndani ya Afrika, kuvutia uwekezaji na kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi. UNDP inaendelea kujitoa kikamilifu kusaidia MSMEs za Tanzania kutumia kikamilifu fursa hizi.”
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, ameeleza kuwa, MSMEs ni sehemu kubwa ya uchumi wa nchi na inahitaji msaada wa pamoja ili kufikia uwezo wao kamili wa kuunda ajira, kuimarisha kipato cha mtu binafsi, na kuchangia zaidi kwenye uchumi wa Taifa.
“Kama CRDB Bank Foundation, tumejizatiti kikamilifu kusaidia ukuaji na ushindani wa SMEs za Tanzania. Kwa uzoefu wetu mkubwa katika kujenga uwezo wa wafanyabiashara, tuko tayari kutoa zana, rasilimali, na mafunzo muhimu ili wajasiriamali wafanikiwe katika soko la AfCFTA. Mpango huu ni hatua muhimu katika juhudi zetu za kuwawezesha SMEs, hasa wanawake na vijana, kupanua biashara zao Afrika nzima na kuleta maendeleo ya kiuchumi,” amesema Tully.
Mwongozo Rahisi wa AfCFTA una lenga kuwa nyenzo muhimu kwa SMEs zinazotaka kupanua masoko yao. Mbali na mwongozo huo, mpango wa kujenga uwezo wa UNDP-CRDB CBF unazidi kuimarisha ushindani wa SMEs na utayari wao kushiriki kwenye biashara za kimataifa.
Kupitia ushirikiano na taasisi muhimu kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), mpango huu unahakikisha kuwa SMEs zinapata msaada unaohitajika ili kushiriki kwa ufanisi katika masoko ya AfCFTA.
Hatua hii ni maendeleo makubwa katika kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kutumia kikamilifu fursa kubwa zinazotolewa na AfCFTA, hivyo kuchochea ujumuishaji wa kiuchumi na maendeleo endelevu barani Afrika.