Unavyoweza kutengeneza pesa kwa kutumia AI

Dar es Salaam. Katika kipindi hiki cha maendeleo ya kasi ya kiteknolojia, teknolojia ya akili mnemba (AI) imeendelea kuwa miongoni mwa uvumbuzi unaobadilisha maisha ya watu duniani.

Teknolojia hii haifanyi kazi tu katika viwanda au kampuni kubwa za kimataifa, bali pia inatoa fursa za kiuchumi kwa watu binafsi katika sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa wataalamu wa teknolojia, kutumia AI kwa usahihi na ubunifu kunaweza kumwezesha mtu kujipatia kipato kikubwa kupitia mitandao au hata katika biashara za kawaida.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM) mtaalamu wa teknolojia ya AI kutoka Sweden, Alexander Morad, aliwahimiza vijana kutoiogopa teknolojia hiyo, bali waiangalie kama nyenzo ya kuongeza ubunifu na kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Katika mkutano huo uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii, Morad alisema kwa kutumia ubunifu katika matumizi ya AI, mtu anaweza kutengeneza fedha kutokana na fursa lukuki zilizopo ndani yake.

Alisema miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na kutoa mafunzo ya matumizi ya AI, kutoa huduma ya maudhui kwa kutumia AI, kufanya uchambuzi wa takwimu na uhariri wa maudhui kutoka ndani na nje ya nchi.

“Unaweza kupata wateja kutoka Ujerumani, Marekani, Sweden na nchi nyingine, ukawasaidia kutatua changamoto zao na kuwapatia huduma mbalimbali kwa kutumia AI kwa bei ambayo kwao ni nafuu sana, lakini kwako ni hela nyingi,” alisema.

“Kwa mfano, kama mtu angeniambia, ‘naweza kuhariri podcast yako, unipe tu dola 150’, ningekubali. Siwezi kumpata mtu Sweden anayefanya hivyo kwa kiasi hicho. Ukipata wateja 10, tayari unapata dola 1,500 kwa mwezi, wakati mshahara wa wastani hapa ni kama dola 230 hadi 300,” aliongeza.

Morad alisema kuwa mtu mwenye ujuzi wa kutosha kuhusu teknolojia hiyo anaweza kufundisha wengine kwa malipo na kujipatia kipato kizuri.

“Ikiwa una ujuzi wa AI, unaweza kuanzisha kozi za mtandaoni, YouTube channel au warsha ambapo watu hulipa ili kujifunza jinsi ya kutumia teknolojia hiyo. Hii ni njia nzuri ya kutengeneza kipato cha mara kwa mara,” alisema.

“Pia unaweza kutoa huduma za ushauri kwa kampuni zinazotaka kuanzisha au kuboresha matumizi yao ya AI,” aliongeza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wadau mbalimbali wa teknolojia, akiwemo Felician Nyanda, ambaye ni mtaalamu wa teknolojia na Mkurugenzi wa kampuni ya BFI.

Nyanda alisema AI siyo tena suala la wataalamu wa kompyuta pekee, kwani mtu yeyote mwenye ubunifu, maono na ujuzi mdogo wa teknolojia anaweza kuitumia kutengeneza kipato.

Nyanda alisema namna AI inavyorahisisha kazi inamwezesha mtumiaji kuhudumia watu wengi zaidi na hivyo kuongeza kipato.

Alitoa mfano wa jinsi AI inavyoweza kutengeneza tovuti na kufanya kazi nyingine nyingi ndani ya muda mfupi.

“Kwa sababu inarahisisha kazi, mtumiaji anaweza kuongeza kipato kupitia kazi anayoifanya kwa msaada wa AI,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM), Leticia Ndongole, alisema taasisi yao imejikita kuhakikisha Watanzania hawabaki nyuma katika mapinduzi ya teknolojia.

“Hatutaki mtu aachwe nyuma, na hiyo ndiyo sababu tumekuwa tukitoa elimu na semina kwa watu wa kada mbalimbali kutumia teknolojia kurahisisha kazi zao,” alisema.

Ndongole alisema kuna umuhimu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya AI kuingizwa katika mitalaa ya elimu ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa mstari wa mbele katika nyanja ya teknolojia.

Kwa wale wenye hofu kuwa AI itapunguza ajira, Ndongole aliwataka kuachana na dhana hiyo kwa kuwa mfumo huo umebuniwa kwa ajili ya kurahisisha kazi na siyo kuharibu ajira.

“Msiichukulie teknolojia kama inakuja kuua ajira zenu. Mnapaswa kutafakari kwa kina na kuja na ubunifu ambao utaitumia teknolojia hiyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *