Unakesha mitandaoni? Basi hii inakuhusu

Dar es Salaam. Kama wewe huwezi kukaa muda mrefu bila kutumia simu yako kuingia kwenye mitandao ya kijamii, upo hatarini kupata tatizo linaloathiri afya ya akili na saikolojia.

Uraibu wa mitandao ya kijamii ni aina ya tabia inayojulikana kwa mtu kuwa na msukumo usiohimilika wa kuingia kwenye mitandao hiyo, wasiwasi kuzidi kiasi na kutumia muda mwingi kiasi kwamba huathiri utendaji wa mambo mengine muhimu ya maisha.

Katika maisha ya sasa ni kawaida watu kutumia muda mrefu kuingia Instagram, X, Facebook, TikTok na mitandao mingine ya kijamii kwa ajili ya kufuatilia taarifa na mambo yanayohusu burudani.

Hata hivyo kupitisha macho kwenye mitandao ya kijamii kumezidi kuwa shughuli maarufu kwa maisha ya kila siku katika muongo uliopita. Ingawa watu wengi huitumia bila matatizo, kuna asilimia ya watumiaji wanaoathirika na kuwa na uraibu wa mitandao hii.

Tovuti ya Addiction Center inasema matumizi ya mitandao ya kijamii kwa hali ya uraibu inaweza kufanana na uraibu wa dawa za kulevya au kamari.

Kwa nini mitandao husababisha uraibu?

Tovuti ya Addiction Center inaendelea kusema uraibu wa mitandao ya kijamii unahusiana na mfumo wa utoaji wa molekuli ya Dopamine katika ubongo.

Dopamine hufanya kazi kwenye maeneo ya ubongo ili kukupa hisia za raha na kuridhika.

Dopamine pia ina jukumu katika kudhibiti kumbukumbu, hisia, usingizi, kujifunza na kazi nyingine za mwili.

Mitandao ya kijamii huanzisha mazingira yanayochochea utoaji wa dopamine kwa njia sawa na dawa za kulevya kama vile kokaini au tabia za uraibu kama vile kamari.

Mitandao ya kijamii imeundwa kwa makusudi ili kuwafanya watumiaji wabaki ndani ya majukwaa hayo kwa muda mrefu iwezekanavyo. Matokeo yake, watu wengi huanza kuonyesha dalili za uraibu kwa mitandao kama vile TikTok, Instagram, Snapchat, Facebook na YouTube.

Tafiti zinaonyesha ‘retweets’, ‘likes’ na ‘shares’ za mara kwa mara huamsha sehemu ya ubongo inayohusika na mfumo kwa njia sawa na dawa za kulevya.

Jinsi mitandao ya kijamii inavyoathiri ubongo

Kutokana na athari zake kwa ubongo, mitandao hii inalevya mwili na saikolojia.  Kwa mujibu wa utafiti mpya wa Chuo Kikuu cha Harvard, kushiriki kwenye mitandao hii hutumia sehemu hiyohiyo ya ubongo inayowashwa wakati wa kutumia dawa za kulevya.

Mtu anapopata kitu cha kufurahisha au neva katika maeneo yanayotengeneza dopamine kwa wingi huwashwa na viwango vya dopamine huongezeka.

Hali hii inaweza kuonekana wazi katika matumizi ya mitandao ya kijamii mtu anapopokea taarifa kama vile like au kutajwa (mention), ubongo hupokea msukumo wa dopamine na kuusambaza jambo linalomfanya kuhisi furaha.

Mitandao na afya ya akili

Vilevile utafiti umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya matumizi ya mitandao ya kijamii, afya mbaya ya akili. Ingawa mitandao ya kijamii ina manufaa yake, matumizi yake kupita kiasi yanaweza kusababisha hisia za huzuni na upweke.

Tafiti za hivi karibuni zimebaini kuwa watumiaji wa mara kwa mara wa mitandao ya kijamii huamini kuwa watu wengine ni wenye furaha na mafanikio zaidi kuliko wao, hasa wanapokuwa hawaijui vyema hali ya maisha yao halisi.

Jambo hilo linaweza kuwa hatari kwa afya ya akili na mtazamo wa mtu binafsi. Matumizi kupita kiasi ya mitandao ya kijamii yanaweza kusababisha kutoridhika na maisha na pia kuongeza hatari ya wasiwasi na huzuni.

Inakadiriwa kuwa asilimia 27 ya watoto wanaotumia mitandao ya kijamii kwa zaidi ya saa tatu kwa siku huonyesha dalili za matatizo ya afya ya akili. Watoto na vijana wako katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika kwa sababu akili zao bado zinakua.

Vijana wanaotumia mitandao ya kijamii tangu wakiwa wadogo hawawezi kuwasiliana vyema ana kwa ana ingawa wanashirikiana mtandaoni.

Tovuti hiyo imeeleza kuwa uraibu wa matumizi ya mitandao husababisha mabadiliko ya kihisia, ufanisi kazini kupungua kwa baadhi ya watu hata katika jamii.

Kukosa uvumilivu wa kukaa bila kutumia mitandao hiyo, kukosa furaha za kihisia na kimwili pale matumizi ya mitandao yanapopungua au kusitishwa.

Kupuuza majukumu ya maisha halisi, kushindwa kuacha kutumia mitandao ya kijamii, hasira au mfadhaiko unapozuiliwa kutumia mitandao ya kijamii, kuelekeza mawazo kwenye mitandao ya kijamii hata wanapokuwa nje ya mtandao pamoja na kupata usumbufu usingizini, ulaji na ratiba za mazoezi.

Akizungumzia athari za matumizi ya mitandao ya kijamii kupita kiasi, Daktari Fabian Maricha amesema inasababisha muhusika kutozingatia muda wa kufanya mambo mengine kwa usahihi.

“Kutopata nafasi ya kujifunza baadhi ya vitu kwa vitendo hasa kwa wanafunzi. Kutengeneza migogoro ya kijamii mfano unakuta mtu anashindwa kumsikiliza mwenzake kiusahihi sababu ya kuzingatia kilichopo kwenye mitandao.

“Kila kitu chenye uraibu athari zake ni  mtu kuwa tegemezi yaani bila hiki siwezi kuwa sawa,” amesema Dk Maricha.

Jinsi ya kuepuka matumizi ya mitandao ya kijamii

Hii hapa ni njia ya kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya mitandao hiyo kupitia simu yako. Hii ni kwa mujibu wa The New York Times.

Kwanza unapaswa kuweka mipaka kupitia mipangilio ya simu kwanza kwa kuzima taarifa ‘Notification’. Kama unatumia iPhone (iOS), nenda kwenye Settings > Notifications na uzime za programu unazotaka.

Katika simu za Android, nenda kwenye Settings > Notifications > App Notifications. Kisha unazima.

Unaweza kutumia mfumo wa ‘Focus Mode” au “Do Not Disturb” ambao utakusaidia kuzuia usumbufu wakati wa kazi au muda mwingine muhimu. 

Pia unaweza kuweka kikomo cha matumizi ambapo kwenye iOS, nenda kwenye Settings > Screen Time > App Limits kuweka muda wa matumizi ya programu. Kwa Android, nenda kwenye Settings > Digital Wellbeing & Parental Controls na uchague programu za kupunguza matumizi. 

Ikiwa bado unajikuta unatumia muda mwingi, jaribu kufuta programu kutoka kwenye simu yako. Kufuta programu hakuondoi akaunti yako, lakini inakufanya uitumie tu kwenye vifaa vingine kama kompyuta mpakato. 

Mtumiaji wa mitandao ambaye ameona haina umuhimu kwake Regina Michael kutoka Dar es Salaam amesema alijiondoa kwenye makundi ya WhatsApp na mitandao mingine kwa kuwa yalikuwa yakimpotezea muda.

“Nilileft magropu zaidi ya 20 mwezi uliopita nikabakiza yale ya kazi niliacha yanayonipa furaha, amani lakini yale ambayo hayana kipya kwangu nilijiondoa.

“Nilifanya hivyo kwa sababu muda mwingi nilikuwa kwenye simu kuliko kufanya kazi manufaa hakuna zaidi ya mawazo,” amesimulia. 

 Amesema kwa sasa amekuwa huru anatimiza majukumu yake ipasavyo kwa kuwa muda mwingi hatumii simu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *