
Takriban raia 500 wamethibitishwa kuuawa huko Darfur Kaskazini mwa Sudani katika wiki mbili zilizopita, Umoja wa Mataifa umesema siku ya Ijumaa, ukilaani idadi “ya kutisha” ya vifo na kuenea kwa unyanyasaji wa kingono.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa imeorodhesha takriban raia 481 waliouawa huko Darfur Kaskazini tangu Aprili 10 na kwamba “idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi”.
Jimbo hilo limekuwa uwanja muhimu wa vita katika vita vilivyozuka Aprili 15, 2023 kati ya jeshi la serikali, linaloongozwa na Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdane Daglo.
Umoja wa Mataifa umesema idadi ya vifo ni pamoja na “raia wasiopungua 210, wakiwemo madaktari tisa” waliouawa katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam kati ya Aprili 11 na Aprili 13.
Pia wamejumuishwa “raia wasiopungua 129” waliouawa kati ya Jumapili na Alhamisi wiki hii katika jiji la El Fasher, wilaya ya Um Kedada na kambi ya watu waliokimbia makazi yao ya Abu Shouk, ofisi ya haki za binadamu imesema katika taarifa.
Aidha, taarifa hiyo imesema, “madazeni ya watu waliripotiwa kufa kutokana na ukosefu wa chakula, maji na huduma za matibabu” katika vituo vya kizuizini vinavyosimamiwa na RSF au “wakati wakitembea kwa siku kadhaa katika mazingira magumu katika jaribio la kukimbia ghasia”.
Vita hivyo vimesababisha makumi ya maelfu ya watu kupoteza maisha na kusababisha kile ambacho mashirika ya misaada yanaelezea kama mgogoro mkubwa zaidi wa kuhama makazi na njaa duniani.
Ofisi ya haki za binadamu imesema mapigano ya Darfur Kaskazini yamewakosesha makazi mamia kwa maelfu ya raia, ambao wengi wao tayari walikuwa wamekimbia makazi yao wakati wa vita.
Waliokimbia makazi yao “wanakabiliwa na hali mbaya huku kukiwa na vizuizi vinavyoendelea vya upatikanaji wa usaidizi wa kuokoa maisha,” imesema.
Ofisi ya haki za binadamu pia imeonya kwamba “mashambulizi ya kikabila yanayolenga jamii maalum” yalikuwa yakitokea tena huko Darfur. Vita huko Darfur vilivyozuka mwaka wa 2003 vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kumekuwa na mashambulizi dhidi ya makabila.
“Idadi inayoongezeka ya majeruhi wa raia na ripoti nyingi za unyanyasaji wa kijinsia ni za kutisha,” Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk amesema katika taarifa.
Ofisi yake, alisema, “ilisikia habari za watu kutekwa nyara kutoka kambi ya IDP ya Zamzam na ya wanawake, wasichana na wavulana kubakwa au kubakwa na genge la watu huko au walipokuwa wakijaribu kutoroka mashambulizi”.
Turk pia ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na wahudumu wa afya.
“Mifumo ya kusaidia wahasiriwa katika maeneo mengi iko kwenye hatihati ya kuharibika, wahudumu w afya wenyewe wako hatarini na hata vyanzo vya maji vimeshambuliwa kwa makusudi,” amesema.
“Mateso ya watu wa Sudan ni magumu kufikiria, ni magumu zaidi kuelewa na haiwezekani kuyakubali.”