
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimetakiwa zizuie hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutekeleza sheria zilizopitishwa na bunge la utawala huo za kuzuia operesheni za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi wa kipalestina, UNRWA ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Ombi hilo limetolewa na Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatano ya Novemba 6, jijini New York, katika kikao kisicho rasmi kilichoitishwa na Rais wa Baraza hilo kumsikiliza Lazzarini.
Akiashiria mauaji ambayo yametekelezwa na utawala haramu wa Israel katika vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Oktoba mwaka jana, amesema hadi leo hii, majengo ya UNRWA yameharibiwa au kusambaratishwa kabisa, na wafanyakazi 239 wa shirika hilo wameuawa.
Amesema vitendo vya Israeli ni vitisho dhahiri kwa UNRWA katika zama za kiza kinene kwa Wapalestina, akisisitiza kuwa “UNRWA ndio nguzo pekee iliyosalia imesimama.”
Mkuu huyo wa UNRWA amesema iwapo Israeli itaamua kutekeleza marufuku hiyo, mamilioni ya wapalestina watatumbukia kwenye zahma.
Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza Kuu kwamba shambulio la moja kwa moja kwenye uti wa mgongo wa juhudi za kimataifa kupitia UNRWA ni ushahidi wa wazi zaidi wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israeli huko Gaz.
Amesema UNRWA ni shirika la kipekee na hakuna kinachoweza kuchukua nafasi yake.