Umoja wa Mataifa jana Jumatatu ulitoa mwito kwa serikali ya Somalia kuongeza uwekezaji katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia nchini humo.
James Swan, Kaimu Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametoa mwito huo na kutaka kupasishwe sheria ya kuharamisha unyanyasaji wa kijinsia kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo Somalia tayari ni mwanachama wake.
“Hii itahakikisha kwamba watu wanaofanya uhalifu watawajibishwa na walionusurika watapata haki zao,” amesema Swan katika taarifa yake iliyotolewa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, mwanzoni mwa kampeni ya kila mwaka ya siku 16 ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia.

Kaulimbiu ya kimataifa ya kampeni ya mwaka huu ni: “Ungana na Wekeza katika Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana.”
Kampeni hiyo pia imetoa mwito kwa serikali zote duniani kushiriki kadiri zinavyoweza kwenye jitihada za kuzuia unyanyasaji wa kijinsia.
Katika sehemu moja ya taarifa yake, Swan amesema: Kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia kunahitaji rasilimali za kifedha na nyenzo, hasa kwa kuzingatia wajibu wa kulindwa wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na jamii za watu wachache ambao wako hatarini zaidi kwa unyanyasaji wa kijinsia.
Vilevile amesema kuwa, katika muda wote wa siku 16, Umoja wa Mataifa nchini Somalia utashirikiana na serikali na asasi za kiraia katika jitihada za pamoja za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na kuharakisha mchakato wa kutungwa sheria za kuwalinda wanawake na wasichana.