UN: Watoto Ghaza hawauliwi na mabomu tu ya Israel, kwa kuzuiwa pia wasiende nje kutibiwa

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema, watoto Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza wanakufa kwa uchungu kwa kukosa matibabu ya dharura kutokana na mamlaka za utawala wa Kizayuni wa Israel kuwazuia wasiende kupatiwa matibabu nje ya eneo hilo lililowekewa mzingiro baada ya kufungwa kivuko cha Rafah.

Kwa mujibu wa mashirka hayo, idadi ya watoto Wapalestina wanaoruhusiwa kupelekwa nje ya Ghaza kwa ajili ya matibabu inazidi kupungua kila siku.

Akizungumzia hali hiyo, Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF James Elder amesema, wakati hapo kabla karibu watoto 300 walikuwa wakihamishwa kila mwezi, idadi hiyo sasa imepungua hadi kiwango cha chini ya mtoto mmoja kwa siku moja, huku madaktari wakikaa bila matumaini yoyote ya kupata idhini kutoka kwa mamlaka za utawala wa Kizayuni wa Israel zinazodhibiti watu kutoka nje ya Ghaza. Ametahadharisha kuwa, ikiwa hali hiyo itaendelea, itachukua zaidi ya miaka saba kuhamisha watoto 2,500 wanaohitaji huduma ya dharura ya matibabu.

James Elder

“Matokeo yake, watoto huko Ghaza wanakufa, sio tu kwa mabomu na risasi na makombora yanayowapiga,” amesema Elder huku akielezea kesi kadhaa za watoto wenye majeraha mabaya yanayohatarisha maisha ambao wamecheleweshwa au kukataliwa kuhamishwa bila kutolewa maelezo yoyote.

Msemaji wa UNICEF ameeleza kwa masikitiko kuwa, hata inapotokea miujiza, wakati mabomu yanaporipuka na nyumba zikaporomoka na idadi kubwa ya watu wakafa, pale mtoto ananusurika, huzuiwa pia asiondoke Ghaza kwenda kupatiwa huduma ya haraka ya matibabu ambayo inaweza kuokoa maisha yake.

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema maisha ya kawaida yanazidi kuwa jinamizi huko Ghaza kwa sababu kukidhi mahitaji ya msingi kama chakula ni mtihani mkubwa kwa watu wengi na kutoa mfano wa hali ilivyo katika mji wa Deir al-Balah ambako hata mkate ambao ni chakula kikuu, kupatikana ni changamoto…/