UN: Wanawake wa Afrika wanatumia masaa milioni 200 kila siku kuteka maji

Wanawake katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, wanatumia masaa milioni 200 kila siku kwa ajili ya kuteka maji.

Hayo yamedokezwa na Jemimah Njuki, Mkuu wa Idara ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, (UN Women) huko Baku, pembizoni mwa  mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29.

Akizungumza na UN News, Bi. Njuki amesema wanawake na wasichana wako hatarini zaidi kukumbwa na ukosefu wa uhakika wa kupata chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameendelea kwa kuonya kuwa: “Uchambuzi wetu tayari unaonesha kuwa katika mazingira mabaya zaidi ya tabianchi, wanawake na wasichana milioni 236 hawatakuwa na uhakika wa chakula, na wanawake na wasichana milioni 158 watatumbukia kwenye umaskini.”

Ripoti ya Hali ya Rasilimali za Maji Duniani iliyotolewa, Oktoba 7 mwaka huu imesisitiza kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hali duni za mtiririko wa mito zimekuwa zikirekodiwa, huku maji yanayofika kwenye  mabwawa yakiwa ya kiwango cha chini. Kupungua kwa usambazaji huo kumeathiri kiasi cha maji yanayopatikana kwa jamii, kilimo, na mifumo ya ikolojia.