UN: Waasi wa Kongo Mashariki waliwateka nyara takriban wagonjwa 130 kutoka hospitali mbili

Waasi wa M23 walioanzisha mashambulizi mashariki mwa Kongo waliwateka nyara takriban watu 130 wagonjwa na waliojeruhiwa kutoka hospitali mbili za mji wa Goma wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa umesema siku ya Jumatatu.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji wa M23 walivamia Hospitali ya CBCA Ndosho na Hospitali ya Heal Africa usiku wa Februari 28, wakichukua wagonjwa 116 na 15 mtawalia, msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani amesema katika taarifa.

Watu hao waliotekwa nyara walishukiwa kuwa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo au wanachama wa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wanaojulikana kwa jina la Wazalendo.

“Inasikitisha sana kwamba M23 inawateka wagonjwa kutoka vitanda vya hospitali katika uvamizi ulioratibiwa na kuwaweka bila mawasiliano katika maeneo yasiyojulikana,” Shamdasani amesema, akitaka waachiliwe mara moja.

Wasemaji wa M23 Willy Ngoma na Lawrence Kanyuka Kingston hawakujibu mara moja kuhusiana na madai haya.

Waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi waliandamana hadi katika mji wa Goma mwishoni mwa mwezi wa Januari na tangu wakati huo wamepiga hatua kubwa kuelekea mashariki mwa Kongo, na kuteka maeneo na kupata madini ya thamani.

Kuendelea kwao, ambapoo ulianza mwishoni mwa mwezi wa Desemba, tayari kunajumuisha ongezeko kubwa zaidi la mzozo wa muda mrefu uliokita mizizi katika kusambaa kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 nchini Kongo na mapambano ya kudhibiti rasilimali kubwa ya madini ya Kongo.

Kongo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo la waasi.

Rwanda inakanusha shutuma hizo na kusema inajihami dhidi ya wanamgambo wanaoongozwa na Wahutu walioazimia kuwaua Watutsi nchini Kongo na kutishia Rwanda.

Takriban watu 7,000 wameuawa mashariki mwa Kongo tangu mwezi wa Januari na karibu watu nusu milioni waliachwa bila makazi baada ya kambi 90 za wakimbizi kuharibiwa katika mapigano hayo, kulingana na serikali.

Vikwazo vya kimataifa, uchunguzi upya wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Afrika yameshindwa kusitisha kusonga mbele kwa waasi, ambao wameiteka miji mikuu miwili ya mashariki mwa Kongo, Goma na Bukavu.