
Wahudumu wa mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa wamelaani mauaji ya zaidi ya watu 3,600 nchini Lebanon katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Taarifa hiyo ambayo imetolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya Lebanon ambayo imeadhimishwa Novemba 22, imesema idadi hiyo ya watu waliouawa katika hujuma ya Israel dhidi ya Lebanon katika miezi ya hivi karibuni inajumuisha zaidi ya watoto 230 huku wengine 15,000 wakiwa wamejeruhiwa.
Ivo Freijsen, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Lebanon amesema “Katika wiki za hivi karibuni, Israel imezidisha kwa kasi mashambulizi yake ya anga na uvamizi wa nchi kavu na hii imeongeza maafa ya kibinadamu ambayo yameathiri raia.”
Ameongeza kuwa wiki chache zilizopita zimekuwa mbaya zaidi na zahma zaidi kwa watu wa Lebanon katika miongo kadhaa.
Hayo yanajiri wakati ambao Kiongozi wa Hizbullah amesema harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon iko tayari kupigana vita vya muda mrefu dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, na kwamba jibu lao kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya anga dhidi ya Beirut litakuwa kulenga katikati mwa Tel Aviv.
Mkuu huyo wa Hizbullah amesema licha ya hali ya machafuko nchini Lebanon, kundi hilo la muqawama litaendelea kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza.