UN: Milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini imeuwa watu 16 Libya tangu kuanza mwaka huu

Watu 16 wakiwemo watoto wadogo wamepoteza maisha huko Libya tangu kuanza mwaka huu wa 2024 kufuatia milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na masalia ya zana za vita ambazo hazikulipuka.

Fatima Zurik Mkuu wa Kitengo cha UNMAS cha Umoja wa Mataifa amesema kuwa zaidi ya mita mraba za ardhi milioni 444 nchini Libya zinahitaji kuondolewa mabaki ya zana za kivita na mabomu ya kutegwa ardhini, akionya kwamba mchakato wa kutegua mabomu hayo unaweza kuchukua hadi miaka 15.

Mivutano kati ya makundi mbalimbali ya wanamgambo imechafua maeneo mengi ya Libya kwa mabomu ya kutegwa ardhini na mabaki ya zana za kivita tangu alipoondolewa madarakani kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi 

Mabomu hayo ya kutegwa ardhini yanaendelea kuuwa watu wasio na hatia huko Libya. 

Nchi hiyo tajiri kwa mafuta imegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu moja inaongozwa na serikali ya mapatano ya kitaifa yenye makao yake huko Tripoli, na nyingine huko Benghazi.