Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imesema kuwa mwaka huu umeshuhudia mauaji ya wafanyakazi wengi wa kutoa misaada ya kibinadamu kuliko mwaka wowote mwingine tangu kuanza kwa takwimu hizi, wengi wao katika mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa Hifadhidata ya Usalama wa Wafanyakazi wa Misaada, ambayo inajumuisha takwimu za matukio ya kuanzia mwaka 1997, wafanyakazi 281 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na hivyo kuvunja rekodi ya awali ya 280 iliyowekwa mwaka 2023.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa, wafanyakazi 178 wa misaada ya kibinadamu waliuawa mwaka huu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ukiwemo Ukanda wa Gaza, ambako kunashuhudiwa mzozo mbaya zaidi kwa Umoja wa Mataifa.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, wafanyakazi 25 wa kutoa misaada wameuawa nchini Sudan.
Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, amesema katika mkutano na waandishi wa habari huko Geneva kwamba: “Watu hawa wanafanya kazi muhimu sana, lakini badala yake wanauawa.”

Ameongeza kuwa wengi kati ya wahanga hao walikuwa wafanyakazi wa ndani, wakati 13 kati yao walikuwa wafanyakazi wa kimataifa wa kutoa misaada ya kibinadamu.
Wafanyakazi wa misaada wanapaswa kupewa ulinzi chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, lakini wataalamu wanasema kwamba kuna mfano michache sana wa kufunguliwa mashtaka ya ukiukaji wa sheria hiyo.