UN imetenga Dolla Milioni 110 kusaidia kuokoa maisha katika mataifa mbalimbali

Umoja wa Mataifa umesema umetenga Dola Milioni 110 kutoka kwa mfuko wake wa dharura ili kusaidia kuokoa maisha ya watu katika mataifa mbalimbali, baada ya makato makubwa yaliyofanywa na serikali ya rais wa Marekani Donald Trump, yaliyokuwa yanatumwa kwa mashirika mbalimbali ya kutoa misaada ya kibinadamu.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Tom Fletcher, Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa, anayeongoza kitengo cha kutoa misaada ya kibinadamu, katika taarifa imesema, fedha hizo zitatumwa katika nchi zinazoathiriwa na vita, mabadiliko ya tabia nchi na hali ngumu ya kiuchumi.

Hatua hii inakuja baada ya hatua ya rais Trump, kuwaathiri mamilioni ya watu duniani, baada ya mashirika ya kimataifa kushindwa kuendelea kutoa misaada mbalimbali.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya Milioni 300 kote duniani kutoka barani Afrika, Asia na Latin America, wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu, baada ya kuathirika kutokana na hatua ya Marekani.

Kwa ujumla mwaka 2025, Umoja wa Mataifa unasema unahitaji Dola Bilioni 45 ili kuwafikia watu Milioni 185 wanaohitaji misaada ya kibinadamu kote duniani, na mpaka sasa imepokea tu asilimia tano ya fedha hiyo.