
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa imesema ripoti zinaonyesha wengi wa wahasiriwa wa mashambulio ya anga ya Israel kwenye eneo lenye wakazi wengi wa Kikristo kaskazini mwa Lebanon walikuwa wanawake na watoto.
Kulingana na wizara ya afya na shirika la msalaba mwekundu nchini Lebanon, takriban watu 21 waliuawa Jumatatu katika shambulio la anga la Israel kwenye mji wa Aitou, wilaya ya Zgharta nchini Lebanon,
Harakati ya muqawama ya Lebanon, Hizbullah, imeapa kuwalinda watu wasio na hatia wa Palestina na Lebanon dhidi ya ukatili wa Israel.
Jeremy Laurence, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Geneva kwamba, “Tunaelewa kuwa ni jengo la makazi la ghorofa nne ambalo lililodondoshewa mabomu. Kwa kuzingatia mambo haya, tuna wasiwasi wa kweli kuhusu kuvunjwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, nalo limeonya kuhusu “kizazi kilichopotea” nchini Lebanon kinachokabiliana na migogoro mingi na ukatili wa Israel.
Kote Lebanon, takribani Walebanon milioni 1.2 wamelazimika kuhama makwao, wengi wao wakikimbilia Beirut na mahali pengine kaskazini katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
Wizara ya Afya ya Lebanon imehesabu idadi ya vifo vilivyotokana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon tangu Oktoba 2023 kuwa ni 2,309.