Umuhimu wa uwekezaji kwenye utafiti wa gesi asilia kufanyika sasa

Umuhimu wa uwekezaji kwenye utafiti wa gesi asilia kufanyika sasa

Katika kila kona ya dunia neno “nishati safi” limekuwa mwangwi unaotangaza matumaini mapya kwa wanajamii.

Kutoka mashamba ya upepo nchini Denmark hadi mitambo ya kuzalisha umeme jua nchini Afrika Kusini, mataifa yanainuka kutokomeza nishati chafu.

China na Marekani wanawekeza katika magari ya umeme, wakati Kenya inazalisha umeme wa joto ardhi, hali inayofanya vijana, wanasayansi na wanaharakati kupaza sauti wakidai mabadiliko.

Miji mingi imeanza kutumia taa za umeme jua, huku vijiji vikifunguliwa kwa mara ya kwanza kupitia vyanzo safi vya nishati ikiwemo ya umeme huku dunia sasa inapigania maisha, ikilinda anga, maji, na hewa.

Tanzania nayo haikuwa nyuma kwani inaendelea na juhudi za kukuza matumizi ya nishati safi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuboresha upatikanaji wa nishati kwa wananchi.

Moja ya kinachofanyika ni kuendelea na ugunduzi na uchimbaji wa gesi asilia iliyopo ili kuhakikisha shughuli nyingi ambazo zilikuwa zinatumia mafuta katika kufanya uzalishaji kama viwanda vihamie katika matumizi gesi ikiwa ni moja ya njia ya kupunguzaji hewa ukaa unaotajwa kuwa na athari katika dunia ikiwemo kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania inakadiriwa kuwa na mita za ujazo trilioni 230 za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.

Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa, mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.

Kwa kipindi cha miaka minne pekee kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025, kiasi cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia futi za ujazo bilioni 301.33.

Kati ya kiasi hicho, futi za ujazo bilioni 142.35 zilizalishwa kutoka Kitalu cha Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 158.98 kutoka Kitalu cha Songo Songo.

Uzalishaji huu ni wastani wa futi za ujazo bilioni 35.59 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 39.74 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.

Kwa kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi ulikuwa wastani wa futi za ujazo bilioni 32.03 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na futi za ujazo bilioni 25.13 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.

Gesi asilia iliyozalishwa ilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme; matumizi ya viwandani, majumbani, taasisi na katika magari.

Kwanini ni muhimu sasa

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo anasema ni muhimu kuhakikisha gesi iliyopo nchini inatumika kikamilifu kwani kuna uwezekano ikapigwa marufuku duniani siku za usoni.

“Hivyo ni vyema kuitumia kabla hili halijatokea,” anasema Profesa Kinyondo.

Alitolea mfano wa katazo ambalo lilikuwa limeanza kuwekwa awali akisema kabla ya vita ya Ukraine utekelezaji wake ulikuwa umeanza kazi lakini baada ya Russia kufunga upatikanaji wa nishati hasa nchi za magharibi ulikuwa mgumu, jambo lililofanya gesi kurudi katika matumizi.

“Na sisi kama nchi tuna kiasi cha kutumia kwa miaka 30, tutakuwa wa ajabu kama hatutaona faida ya kutoitumia sasa hivi. Mpaka sasa kuna sehemu ambayo imegunduliwa lakini kuna maeneo ambayo yana uwezekano wa kuwa na nishati ya kutosha ikiwemo katika maeneo ya bonde la ufa,” anasema.

Kwa saa gesi bado inaonekana kuwa nishati safi ukilinganisha na aina nyingine za nishati nyingine kama mafuta huku urahisi katika upatikanaji wake, uwepo wake nchini ukiweka urahisi zaidi.

“Pia, ni muhimu sana kuitumia kwani katika utengenezaji wake tunapata bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea,” anasema.

Mchambuzi wa uchumi, Oscar Mkude anasema ni muhimu kutumia gesi asilia iiyopo nchini kwa sasa lakini kama nchi itashindwa kuifungamanisha na uchumi faida ambayo inatajwa itakuwa ngumu kuonekana.

Hiyo ni kwa sababu mbali na gesi kutumika kama nishati kwenye mitambo ya uzalishaji viwandani, pia, inaweza kutumika kama mbolea inayoweza kuinua kilimo nchini.

“Kwenye kuzalisha mbolea ndiyo msingi mkubwa kwa sababu Tanzania tunategemea kilimo na nchi zinazotuzunguka wanategemea kilimo, ukiweza kuzalisha mbolea kwa kutumia gesi yako utatosheleza uhitaji wa ndani na kuuza kwa jirani zako kwa wingi hii ni hatua ya kwanza kuelekea uzalishaji mazao kwa kiwango kikubwa,” anasema.

Utumiaji wa mbolea ni chini ya wastani nchini ni moja ya changamoto ambayo inatajwa kwani wakulima wa Tanzania hawajaweza kufikia hata kiwango cha Afrika mashariki.

Uwekezaji utakaosaidia uzalishaji mbolea utasaidia kufungamanisha kilimo na sekta ya viwanda kwani itasaidia kurahisisha upatikanaji wa malighafi hali itakayofanya viwanda vifanye kazi kwa kiwango kinachotakiwa.

“Ukiwa na uhakika wa kulima mwaka mzima, viwanda vitaondoa wasiwasi wa kupata malighafi, hakuna kiwanda kinachotaka kufanya uzalishaji kwa miezi michache mingine afunge kwani itakuwa ni hasara,” anasema.

Hata hivyo, anasema ni muhimu kuhakikisha uzalishaji gesi unaendana na uwekezaji katika maeneo mengine ili kutengeneza uhakika soko kwa wawekezaji.

Nini kinafanyika

Wakati hayo yakisemwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) inasema iko katika maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambapo kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2013.

Kunadiwa kwa vitalu hivyo kunalenga kutafuta wawekezaji watakaopewa maeneo kufanya shughuli za utafutaji mafuta na gesi kupitia utaratibu wa mikataba ya kugawana mapato (PSA) ambayo huingiwa kati ya Serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za kimataifa za nishati (IECs).

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni anasema Serikali imeamua kunadi vitalu hivyo kwa kutambua umuhimu wake kwa ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Amesema wanatumia njia ya kuita wawekezaji katika sekta hiyo kwani inahitaji fedha nyingi huku akitolea mfano wa kuchimba kisima kimoja nchi kavu gharama yake ni takribani Dola za Marekani 20 milioni (Sh 53.82 bilioni) huku kisima cha baharini gharama yake ikiwa ni dola 80 milioni (Sh216.4 bilioni).

“Na kuna wakati baharini tulichimba kwa dola milioni 175 (Sh473.38 bilioni) na hatukupata kitu. Mpaka sasa Tanzania tumeshachimba visima 96 na 44 kati yake ndiyo tulipata gesi 52 tulitoka patupu.

“Unaweza kuona ni ngumu kiasi gani kwa Mtanzania kumwambia aweke dola 20 milioni za Marekani (Sh53.82 bilioni) au TPDC halafu akute kavu wakienda bungeni watagawanya fedha zilizotumika kwa idadi ya zahanati ambazo wangeweza kujenga,” anasema.

Anasema jambo hilo ndiyo sababu ya kuziachia kampuni kuhusika na utafutaji kwa sababu baadhi yao wanazo sehemu za kufidia huku akifafanua zaidi kuwa huenda wamewekeza maeneo mengine kama uarabuni.

“Na kampuni zilizowekeza huko unakuta labda walichimba uarabuni ambapo wakati huo uchumi ulikuwa unaonyesha kuwa mafuta yatauzwa labda kwa lita Sh300 watarejesha fedha lakini hadi kufikia wakati wanaogundua wanakuta bei imefika Sh600, ile fedha ya ziada wanaweza kuleta huku waendelee na ugunduzi,” anasema Sangweni.

Kwa mujibu wa mikataba ya PSA, mwekezaji hutumia fedha zake katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambapo akikosa huwa anarudisha eneo kwa Serikali na kuondoka.

Lakini, akipata mafuta au gesi asilia, fedha zipatikanazo baada ya mauzo ya rasilimali iliyopatikana hulipa mrabaha, hurudisha mtaji aliowekeza, hulipa kodi na tozo mbalimbali na kinachobaki hugawiwa kwa wabia wa mkataba ikiwemo Serikali na TPDC.

Akizungumzia sababu ya vitalu hivyo kutopata wateja tangu viliponadiwa kwa mara ya mwisho mwaka 2013, Sangweni anasema baada ya kutangazwa kwake, mwaka 2014 bei ya mafuta ilishuka kutoka dola 100 hadi dola 30 kwa pipa.

“Hali hiyo ilifanya wawekezaji wakakosekana, pia ujio wa sheria mpya ulileta mkanganyiko hasa asa walipotaka kufanyiwa mapitio.Ila kupitia hili waliimarisha miundombinu yao ya kisheria na kiusimamizi kwani moja yua malalamiko ya wawekezaj kuwa tpdc ni mdau katika utafutaji na ndiyo msimamizi ndiyo maana pura ikaanzishwa kama chombo huru,” anasema.

Wakati wa uongozi wa awamu ya tano, kwa mujibu wa Sangweni, kulitolewa maagizo ya kutaka kufanywa mapitio ya mikataba ya kugawana mapato (PSA) kwani zilizokuwapo ilidaiwa kuwa hazikuingiwa vizuri.

Hali hiyo ilifanya Bunge kuridhia kufanywa mapitio hayo, hivyo Mwanasheria Mkuu alipewa kazi lakini ilipofika awamu ya sita waliamua kubadilisha muundo na waliendelea na kazi kwa sababu dunia inahama huku wakihofia kuwa utafika wakati gesi itakuwa kama makaa ya mawe.

“Tuliamua twende kwa kasi tuitoe gesi tuitumie hata kikanda tupate thamani ya kile tulichonacho hata dunia ikihama tuwe tumeshahama,” anasema Sangweni.

Hata hivyo, hayo yote yanafanyika huku wakiangalia yaliyokwamisha hilo kufanikiwa kwa wakati ule, wanaboresha ikiwemo mabadiliko ya kisheria yaliyotokea kwa wakati huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *