
Katika dunia ya sasa inayosukumwa na maendeleo ya teknolojia, ujuzi wa kidijitali umekuwa moja ya mahitaji muhimu katika maisha ya kila siku. Sekta mbalimbali zinapitia mageuzi makubwa ya kidijitali, na wale wasioweza kuendana na mabadiliko haya wanajikuta wakiachwa nyuma.
Si kazini, tasisi za utoaji elimu, nyumbani; mwote humo ujuzi wa kidijitali unatajwa kuwa mhimili muhimu wa kuleta mafanikio.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ( WB), karibu asilimia 70 ya kazi mpya katika maeneo mbalimbali duniani, zinahitaji angalau ujuzi wa msingi wa kidijitali. Hii inamaanisha kuwa wafanyakazi wasio na maarifa haya wanakabiliwa na changamoto ya kushindana katika soko la ajira linalozidi kubadilika kwa kasi.
Miaka miwili iliyopita wakati wa kongamano la dijitali barani Afrika, Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Smart Africa, Lucina Kone alisema kuwa katika ulimwengu huu wa sasa kila kampuni ni kampuni ya kidijitali.
Alisisitiza kuwa teknolojia ya dijitali sio tu ni kitu muhimu lakini ndiyo kila kitu kwa kila taasisi inayotaka kuwa na ufanisi ulio bora.
Kwa hali ilivyo sasa, ujuzi wa kidijitali si jambo la hiari tena bali ni hitaji la msingi kwa wafanyakazi na hata kwa wale wanaotafuta ajira. Serikali, sekta binafsi, na taasisi za elimu zinapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa watu wanapata mafunzo ya kutosha ili waweze kuendana na mabadiliko haya.
Dijitali ni ushindi
Katika ulimwengu unaoongozwa na teknolojia, wale watakaowekeza katika maarifa ya kidijitali ndio watakaokuwa washindi wa sasa na kesho.
Katika mazingira ya kazi, teknolojia imekuwa mhimili mkuu wa ufanisi. Kampuni nyingi sasa zinatumia mifumo ya kidijitali kurahisisha shughuli kama vile mawasiliano, usimamizi wa rasilimali watu, na upangaji wa miradi.
Kwa mfano, mfanyakazi anayejua kutumia Excel anaweza kuchanganua takwimu kwa haraka na kutoa uamuzi sahihi, tofauti na yule anayelazimila kufanya kila kitu kwa njia ya ukokotozi wa kawaida. Vilevile, wafanyakazi wanaojua kutumia mifumo ya mawasiliano kama Zoom, Slack au Microsoft Teams, wanaweza kushirikiana kwa ufanisi hata wanapofanya kazi wakiwa maeneo tofauti. Umbali hakuna tena nafasi mbele ya teknolojia.
Jitihada zilizopo
Kutokana na umuhimu wa ujuzi wa kidijitali katika maisha ya kila siku, Serikali na taasisi mbalimbali zimefanya juhudi za kuongeza uelewa wa masuala ya kidijitali miongoni mwa watu hususani vijana ili kuwa na mustakabali ulio bora.
Mathalani, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania inaeleza kuwa mpaka sasa imefanikiwa kutoa ujuzi wa kidijitali kwa wasichana zaidi ya 3,000 hapa nchini kupitia programu yao ya Code like a girl.
Miongoni mwa wanufaika wa programu hiyo ni Nasra Majid, anayesema sasa anaweza kutengeneza ‘
tovuti na anaamini kazi hiyo itamfanya apate pesa ya mtaji wa kufungua biashara.
“Kupitia maarifa ya dijitali niliyoyapata nitaweza pia kutangaza hata hiyo bishara yangu ili kuwafikia wateja wengi zaidi,” anasema mwanafunzi huyo wa shahada ya ugavi katika Chuo cha Uhasibu (TIA).
Nasra ambaye ni mlemavu wa kusikia (kiziwi) anasema ujuzi wa kidijitali, unamsaidia hata katika masomo yake kwani hurahisisha mawasiliano, huku baadhi ya kazi zake za chuo anasema pia huzifanya kwa kutumia kompyuta ambayo kumrahisishia katika kutafuta mawazo mbadala.
Umuhimu wa ujuzi wa kidijitali kazini
Akizungumza na wanufaika wa Code like a girl,Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Vodacom Vivienne Penessis anaeleza kuwa ujuzi wa kidijitali ni muhimu kwani kwa sasa huwezi kufanya kazi kwa tija bila kuwa nao
“Fikiri kwa mfano leo nataka kuandika barua kwenda kwa watu 20, nitaandika barua moja baada ya nyingine lakini kwa kutumia dijitali nitaandika moja kisha nitaituma kwenye barua pepe ya kila mtu kwa mkupuo au hata kuweka kwenye jukwaa la kidijitali ambalo kila mtu anaweza kulifikia,” anasema.
Penessis anasema jambo lingine kuhusu dijitali ni kuwa ukitumia njia zake, ujumbe au kazi yako inafika ulimwengu mzima tofauti na mbinu za kizamani ambazo zitafikia watu wachache.
“Kwa kutumia dijitali unaweza kufikia mamilioni ya watu ambao bila dijitali usingedhani kuwa ungeweza kuwafikia. Uzuri wa dijitali pia inatunza kumbukumbu kirahisi, muda wowote unaweza kutafuta unachokitaka na ukapata taarifa yake kwa urahisi,” anasema.
Kuhusu neema zilizoletwa na dijitali, Penessis anasema ni kuifungua dunia kwa kila mtu kuweza kujifunza na kupata taarifa nyingi bila kuhitaji kusafiri kwenda sehemu mahususi au kumjua mtu fulani.
Nikihitaji taarifa za kijinsia, idadi ya watu, ninachotakiwa kufanya ni kuingia katika mtandao tu na ukweli ni kwamba kwa dunia ya sasa, huwezi kusonga mbele bila kutumia dijitali kwa sababu kila tunachokifanya kinahusiana na dijitali.
Anasema ndiyo maana Vodacom ikaanzisha programu hiyo ya Code like a girl, akisema kinachofundishwa Tanzania ni sawa na ambacho wanafundishwa mabinti wa nchi kama Italia, Hisipania na katika masoko mengine ya Vodacom.
Anasema kama mkuu wa idara ya rasilimali watu, suala la ujuzi wa kidijitali ni miongoni mwa masuala muhimu wanayozingatia wakati wa kuajiri, kwa kuwa ni jambo muhimu katika kazi za kila siku.
“Uzuri ni kwamba ili uajiriwe kwetu lazima uwe umepitia mchakato wa kidijitali, kwakuwa tukitoa tangazo la kazi mtu anafanya maombi kidijitali, na mchujo wa awali unafanywa na kompyuta kwa kuangilia majukumu ya kazi na kati ya walioomba ni wangapi wanaweza kuyamudu, ” anaeleza.
Anasema uzuri wa dijitali unaondoa ubaguzi kwa kuwa mchakato wa kompyuta haukuonyeshi hata jina la mwombaji, badala yake kunatumika herufi za mwanzo za majina yake hivyo kila mtu anapewa haki sawa.
” Kompyuta inatupunguzia hata kazi sisi, maana ajira zetu ukitangaza unaweza kukuta wameomba watu 2,000, fikiria mtu mmoja apitie maombi yote, lakini ukienda kidijitali kompyuta inatumia dakika moja kuchuja wasifu na kukupa wachache wa kuwasiliana nao,” anasema.
Anaongeza kuwa hata hatua zinazofuata ikiwemo za kuitwa kwenye usaili, nazo zinafanyika kwa njia ya dijitali ikiwemo barua pepe na simu.
Mageuzi ya kidijitali na mustakabali wa ajira
Tafiti zinaonyesha kuwa ajira nyingi za kitamaduni zinapotea huku nafasi mpya za kazi zikiibuka katika sekta za teknolojia, biashara kimtandao na huduma za mtandaoni.
Kwa mfano, kazi za uhasibu na utawala ambazo awali zilihitaji takwimu kufanywa na binadamu, sasa zinaweza kufanywa na programu maalum za kompyuta.
Nchini Tanzania, benki nyingi sasa zinahama kutoka huduma za moja kwa moja hadi huduma za mtandao, ambapo mteja anaweza kufanya miamala yake kupitia simu janja au kompyuta. Hili linaonyesha kuwa wafanyakazi wa sekta hiyo wanapaswa kujifunza teknolojia mpya ili kuendana na mabadiliko hayo.
Mbali na kusaidia ufanisi mahali pa kazi, ujuzi wa kidijitali unafungua milango ya fursa za kiuchumi.
Katika ulimwengu wa sasa, watu wanaweza kufanya kazi kwa njia ya mtandao bila kujali walipo.
Mfano mzuri ni watu wanaofanya kazi za uandishi wa maudhui, ubunifu wa picha, au uuzaji wa bidhaa kupitia mitandao ya kijamii.
Vijana wengi sasa wanajiajiri kwa kufanya kazi za mtandaoni kama vile biashara za kimtqndao ( e-commerce), kutengeneza programu na tovuti au kufanya masoko kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, na TikTok