Umuhimu wa mabadiliko madogo ya Katiba kabla ya uchaguzi mkuu

Umuhimu wa mabadiliko madogo ya Katiba kabla ya uchaguzi mkuu

Katika mjadala wa kisiasa wa sasa nchini Tanzania, dhana ya “mabadiliko madogo ya Katiba,” imezua mjadala mkubwa, hasa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuibua kauli mbiu ya No Reforms, No Election (NRNE).

Katika kampeni hiyo, chama hicho kikuu cha upinzani nchini, bado kimeendelea kusisitiza kuwa kama Serikali haitakubali kufanya marekebisho ya msingi ya Katiba, uchaguzi mkuu hautakuwa halali.

Mabadiliko madogo ya Katiba siyo muhimu tu kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki unafanyika, bali pia kuufanya uwe halali kikatiba. Kwa mujibu wa Ibara ya 64(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria.

Hata hivyo, Ibara ya 64(5) inasema Katiba ina nguvu ya juu zaidi ya sheria zote, na kama sheria yoyote itakiuka masharti ya Katiba, basi sheria hiyo ni batili kwa kiwango inachokiuka Katiba.

Mfano hai ni kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kupitia Sheria Na. 2 ya Mwaka 2024, bila kufanya marekebisho ya Katiba kuifuta NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) na kuingiza rasmi INEC.

Katiba bado inaitambua NEC kama chombo halali na hivyo sheria hiyo mpya ni batili hadi pale Katiba itakaporekebishwa rasmi.

Sheria batili kisheria huitwa null and void ab initio, yaani haina nguvu tangu mwanzo.

Kifungu cha 4 cha Sheria Na. 2 ya 2024 kinasema Tume hiyo mpya (INEC) imeundwa chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba.

Lakini ibara hiyo inaitaja NEC, siyo INEC. Kwa mantiki hiyo, kuhalalisha uwepo wa INEC kunahitaji mabadiliko madogo ya Katiba ili kubadilisha jina hilo na kuiondoa NEC.

Aidha, Ibara ya 98(1) na (2) ya Katiba inasimamia mabadiliko ya Katiba, na hairuhusu kubadilisha vipengele vya Katiba kwa kutumia sheria ya kawaida. Hivyo, Bunge haliwezi kutumia sheria ya kawaida kubadili jina la Tume ya Uchaguzi bila kupitia utaratibu wa kikatiba.

Katika historia, kati ya mwaka 1979 na 2005, Bunge lilifanya mabadiliko ya Katiba mara 14 kwa njia isiyo halali, kwa kutumia sheria za kawaida badala ya utaratibu maalumu wa kikatiba.

Uzoefu huu wa “kuyazoea ya kunyonga” ndio unasababisha sasa kufanya kosa hilo tena kwa kuanzisha INEC kabla ya kubadili Katiba.

Kwa kuwa bado muda upo kabla ya uchaguzi mkuu, mabadiliko haya madogo yanaweza kufanyika kwa dharura, ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa kikatiba, halali na wa haki. Rais ana mamlaka, kupitia ushauri wa wataalamu wa sheria kama vile kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kufanya marekebisho haya kwa busara na hekima alizoonyesha kupitia ajenda yake ya 4R.

Tukifanya hivyo, tutaepusha migogoro isiyo ya lazima, uchaguzi utakuwa huru na halali na taifa letu litapata heshima kitaifa na kimataifa.

Rais Samia atakuwa ameandika historia ya dhati ya utawala wa sheria na haki, na Watanzania watabarikiwa kwa taifa lenye utulivu na demokrasia ya kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *