Dar es Salaam. “Kufua shuka mpaka nione linabadilika rangi, kitu pekee ninachoheshimu ni foronya ya mto hiyo baada ya siku kadhaa huwa nahisi inatoa harufu, kwa kuwa huchafuka haraka kuliko shuka,” hiyo ni kauli ya kijana Omary Juma, akielezea anabadilisha shuka baada ya siku ngapi.
“Nakumbuka nikiwa shule tulilalia mashuka mpaka siku ukifua unalala usingizi mzuri kwa kuwa unaona hata hewa inabadilika.”anasema.
Omari (28) ni miongoni mwa vijana wasiooa, maarufu ‘mabachela’ ambao wamezoea kulalia mashuka na mito kwa muda mrefu pasipo kufua.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema ni muhimu kufua na kupiga pasi mashuka kila baada ya wiki moja, utafiti uliofanyika na kampuni ya vitanda ya Marekani ya Amerisleep, umebaini foronya isiyofuliwa kwa wiki moja ina takriban bakteria milioni tatu kwa kila nchi ya mraba, takriban mara 17,000 zaidi ya bakteria waliopo kwenye sinki la choo.
Baadhi ya wanaume waliozungumza na Mwananchi, walisema wamekuwa na mazoea ya kulalia shuka mpaka wahisi linatoa harufu au linabadilika rangi, ndipo huchukua maamuzi ya kulifua.
Abuu Kizigo (30) anasema amekuwa akipitisha hata wiki mbili pasipo kufua shuka na wakati mwingine hulitoa baada ya kuona limechafuka.
“Siyo nafua fua tu, sisi watoto wa kiume kufua ni kama Mchaga na taarabu na ndiyo maana wengine wanakimbilia kuoa.

“Mimi kufua wakati mwingine likitoa harufu, napitiliza hata wiki inaisha niseme tu siku 20 nimeshawahi kulala na shuka bila kufua ndiyo maana wanaume wengi hatunaga mashuka mengi hasa tukiwa mabachela, na hata rangi inakua si nyeupe unatafuta angalau shuka la zambarau, njano, lenye mistari mistari,” anasema Abuu huku akicheka.
Anaongeza, “Nikienda kwa washikaji zangu unalala unasikia shuka inatoa harufu, kila geto mara nyingi lina harufu na ukitafuta sababu ni mashuka au soksi.”
Juma Abdalah (26) anasema, “Hakuna kitu kinanitesa kama kufua shuka, nikililalia nikiwa na jasho tu ninalifua lakini inategemea, wiki moja na nusu hivi au mbili, mimi kufua sio shida kuanua nguo kipengere sana.”
Hali ni tofauti na wanawake ambao hawajaolewa, ambao wanasema wamekuwa wakilala na shuka kwa siku mbili hadi tatu ndipo huzifua.
“Huwa ninabadilisha mashuka kila baada ya siku mbili, sasa suala la kuyafua hilo ni jambo jingine ninaweza kuziweka hata shuka tano ndipo nikazifua,” anasema Janeth Swai (23).
Jamila Ally (45) anasema ana utaratibu wa kubadilisha shuka kila baada ya wiki moja ingawa mwenza wake ambaye anaishi mbali akirudi nyumbani huyatoa kila baada ya siku tatu.
Kwa mujibu wa Dk Isaya Mhando amesema utaratibu mzuri ni kubadilisha shuka kila baada ya wiki moja kwa kuwa tayari huwa limechafuka kwa jasho, takataka zingine za mwilini hata kama muhusika ataona bado ni safi.
Kwa mujibu wa Dk Mhando ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, amesema kufua shuka ni jambo binafsi sana na wengi wamekuwa wakilipuuzia ni kama kufua soksi na boksa kwa wanaume.
“Umelalia shuka hata kama ni siku tatu mwili unatoa jasho, kipindi hiki cha joto unaamka asubuhi umechoka ukikaa muda mrefu bakteria wataendelea kuzaliana pale. Kawaida ukilalia shuka angalau badilisha kabla wiki haijaisha.
“Cha msingi liwe kavu na safi. Wakati wa baridi na joto kuna watu hutokwa na jasho lazima libadilishwe na hakikisha unapolifua lipige pasi, ndiyo maana kwenye nyumba za wageni lazima wabadilishe shuka kila siku.”
Kwa mujibu wa Dk Mhando shuka likipigwa pasi vimelea vingine vinakufa, na ndiyo sababu baadhi ya watu huamka kichwa kinauma kwa kuwa chumba walicholala hakikuwa na oksijeni ya kutosha.
Jambo la kuogofya kuhusu kitanda chako ni kwamba kuna mamilioni ya bakteria, fangasi, wadudu na virusi ambao wanakua sehemu yenye joto palipojaa jasho, mate, chembechembe za ngozi zilizokufa na ndio chakula kwa ajili yao.
Kwa bahati mbaya, vidudu hivyo na mabaki yake (kinyesi) vinaweza kusababisha mzio, pumu na ukurutu.
Mashuka ya kitanda ni kimbilio la bakteria pia. Mito na shuka zilizo na unyevunyevu kutokana na jasho hutoa mazingira bora kwa baadhi ya bakteria na fangasi kuzaliana.
Mwaka 2013, kampuni ya vitanda ya Marekani ya Amerisleep ilichukua sampuli kutoka katika foronya ambayo haikuwa imefuliwa kwa wiki moja ambapo ilikutwa na bakteria milioni tatu kwa kila nchi ya mraba – takriban mara 17,000 zaidi ya bakteria waliopo kwenye sinki la choo.
Mwaka 2006, Denning na wenzake walikusanya mito sita kutoka kwa marafiki na familia. Mito hiyo ilikuwa ikitumika mara kwa mara na ilikuwa na umri wa kati ya miezi 18 na miaka 20. Mito yote ilikuwa na fangasi, hasa aina ya Aspergillus fumigatus ambao hupatikana kwa wingi kwenye udongo.
“Unazungumza mabilioni au matrilioni ya chembe za fangasi kwenye kila mto,” amesema Denning.
“Chanzo cha kupatikana fangasi wengi ni kwa sababu wengi wetu tunatokwa na jasho usiku. Pia, sote tuna wadudu wa vumbi vitandani mwetu na kinyesi cha wadudu hao hutoa chakula kwa fangasi. Na kisha jioni mto hupata joto kwa sababu kichwa chako hulala hapo, kwa hivyo kuna unyevu, chakula na kuna joto.”

Amesema kwa kuwa wengi wetu huwa hatufui mito yetu, fangasi huishi katika hali ya utulivu na wanaweza kuishi kwa miaka. Hata kama hutofua foronya, fangasi wanaweza kuishi katika halijoto ya hadi nyuzi joto 50C (122F).
Mazingira hayo yana athari za kiafya kwa watu wenye ugonjwa wa kupumua, haswa pumu na maambukizi kwenye pua.
Takriban nusu ya watu walio na pumu kali wana mzio na vimelea vya Aspergillus fumigatus, vinavyoweza kusababisha ugonjwa sugu wa mapafu kwa watu ambao hapo awali waliugua kifua kikuu au ugonjwa wa mapafu unaohusiana na uvutaji sigara.
Kwa mujibu wa Denning, asilimia 99.9 ya watu walio na mfumo mzuri wa kinga ya mwili wanaweza kustahimili kuvuta vimelea hivyo, kwa walio na kinga dhaifu, fangasi hao wanaweza kuuzidi nguvu ulinzi dhaifu wa mwili na kusababisha maambukizi.
“Ikiwa una saratani ya damu, au umepandikizwa kiungo au uliwahi kupata madhara ya Uviko-19 au mafua kwa muda mrefu, vimelea hivyo vinaweza kuingia kwenye mapafu na kuendelea huharibu tishu za mapafu,” amesema Denning.
Pamoja na utafiti huo, wataalamu mbalimbali katika mitandao ambayo Mwananchi ilipitia wameonyesha kuwa muhimu kufua shuka na foronya zinazotumika kitandani kila baada ya wiki moja. Pia wamesisitiza ni muhimu kuzipiga pasi kabla ya kuzitumia tena ili kupunguza idadi ya bakteria.