Umuhimu na matokeo ya kuchaguliwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah nchini Lebanon

Miwezi mmoja baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imemchagua Sheikh Naim Qasim kuwa Katibu Mkuu mpya wa harakati hiyo ya muqawama.

Sayyid Hassan Nasrallah aliuawa shahidi tarehe 27 Septemba katika kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa Lebanon. Siku 33 baada ya jinai hiyo, Sheikh Naim Qassem mwenye umri wa miaka 70, ambaye hapo awali alikuwa naibu wa Sayyid Hassan Nasrallah, amechaguliwa katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon. Kuchaguliwa kwa Sheikh Naim Qassem kama Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah nchini Lebanon ni muhimu kwa sababu kadhaa.

Sababu ya kwanza ni kwamba Sheikh Naeem Qasim ana historia ndefu ya utendaji katika harakati mbili za mapambano za Amal na Hizbullah. Ni mmoja wa waasisi wa harakati hizo nchini Lebanon.

Sifa hii muhimu ya inamfanya Sheikh Naim Qassem kuwa na uwezo mkubwa wa kuunda upya na kuimarisha nguvu za kimuundo na kijeshi za Hizbollah. Hassan Ebrahim, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anasema kuwa chaguo hili limetokana na haiba ya Sheikh Naim Qasim. Sheikh Qasim ni mchamungu na mtendaji katika idara za harakati hiyo na ana shakhsia makini na imara.

Suala la pili la umuhimu wa kuchaguliwa Sheikh Naim Qassem kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah nchini Lebanon ni kwamba, jambo hilo linaonyesha wazi kuwa licha ya jinai za utawala wa Kizayuni na mauaji ya idadi kubwa ya makamanda na viongozi wa Hizbullah, lakini harakati hiyo bado ina nguvu kubwa kimfumo na kijeshi, na kwamba sasa imeondokana na mshtuko mkubwa ilioupata kutokana na mauaji ya kiongozi wake shupavu na mwenye haiba, Sayyid Hassan Nasrallah.

Shahid Hassan Nasrullah

Kuchaguliwa Katibu Mkuu kunaonyesha mshikamano na uthabiti wa ndani katika harakati ya Hizbullah na Baraza Kuu lake la uongozi. Suala la tatu la umuhimu wa kuchaguliwa Sheikh Naim Qassim kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah ya Lebanon ni kwamba inaonesha kuwa harakati hii itaendelea kupigana dhidi ya utawala wa Kizayuni na kulichukulia jambo hilo kuwa moja ya sera zake kuu. Shakhsia ya Sheikh Naim Qasim na tajriba yake ya kuwa naibu katibu mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kwa zaidi ya miaka 30, pamoja na tajriba ya kushiriki kwake katika vita vinne vya miaka ya 1993, 1996, 2000 na 2006, ni mambo yanayoonyesha kuwa Hizbullah katika kipindi cha uongozi wa Sheikh Naim Qasim itaendeleza njia ya Sayyid Hassan Nasrallah katika mapambano dhidi ya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu na kuchukua hatua muhimu katika mhimili wa muqawama.

Nukta ya mwisho ni kwamba, kuchaguliwa Sheikh Naim Qassem kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah nchini Lebanon katika hali ambayo utawala wa Kizayuni unawaua kigaidi viongozi na makamanda wa harakati hiyo, kunaonyesha kuwa viongozi na makamanda wa Hizbullah si tu hawaogopi jinai na ugaidi wa utawala huoi, bali wameazimia vilivyo kuendeleza njia ya jihadi, mapambano na shahada wakiwa na mwamko kamili. Na hili ndilo suala la msingi ambalo utawala wa Kizayuni umeshindwa kulidiriki, na ndio maana unaendelea kuwaua kigaidi viongozi na makamanda wa Hizbullah na makundi mengine ya muqawama ukidhani kuwa jinai hizo huenda zikasimamisha na kuzima moto wa mapambano dhidi ya dhulma na ukandamizaji wake katika eneo.