Umoja wataja kuboresha mifumo ya chakula

Unguja. Ili kutekeleza mipango ya kuboresha mifumo ya chakula nchini, Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na wadau wengine wametakiwa kufanya kazi pamoja ili kuleta mabadiliko chanya tofauti na ilivyo sasa kila mmoja anafanya kazi kivyake.

Hayo yamebainika leo Aprili 26, 2025 katika mkutano uliowaleta pamoja wadau wa mfumo wa chakula Zanzibar.

Wamesema kila mmoja anapaswa kuwa balozi kuhakikisha mifumo ya chakula inazingatiwa badala ya kuachia sekta moja.

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa, la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Deborah Esau amesema sekta zinazohusika kuboresha afya na lishe kila moja inafanya kazi kivyake jambo ambalo haliwezi kuleta matokeo chanya.

“Tanzania iliingia makubaliano ya kuboresha huduma ya chakula ili iweze kuleta mabadiliko chanya kwa watu wake, hata hivyo bado sekta nyingi hazijakaa vizuri kila moja inafanya kazi kivyake,” amesema.

Amesema lengo la mkutano huo ni kuleta uelewa wa pamoja kwa wadau wanaohusika na mifumo ya chakula, kushirikiana na kuleta mabadiliko chanya katika utekelezaji wa mifumo inayohusu chakula.

“Lazima tuache kufanya kazi kila mtu peke yake, tushirikiane kuweka mikakati ambayo itatusaidia kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha mlaji wa mwisho ananufaika na kuwa na mifumo ya chakula ambayo ni himilivu na stahamilivu,” amesema.

Mkuu wa Divisheni ya Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Kilimo, Zainab Hassan Moyo amesema wizara ina mambo kadhaa inafanya katika kutekeleza usalama wa chakula, ikiwamo kuwa na miradi ya kilimo, misitu, mifugo na kuangalia afya ya udongo.

Akizungumzia changamoto katika mfumo wa chakula amesema ipo katika bajeti, kwani inayowekwa ni nzuri lakini wanashindwa kutekeleza kutokana na kima cha fedha wanachopatiwa kinakuwa kidogo na miradi mingi wanashindwa kuitekeleza.

Ofisa mwingine wa wizara hiyo, Muhamed Mwinyi Hassan amesema wizara inatarajia kuwa na kilimo cha umwagiliaji katika eneo la ekari 8,521 ifikapo mwaka 2050. Kwa sasa eneo linalohusika na umwagiliaji ni ekari 2,300.

Kuhusu mbolea amesema inayopatikana ni tani 2,700 katika msimu mmoja.

Ofisa lishe kutoka Wizara ya Afya, Khalid Abdi amesema wizara imeweka mikakati ikiwamo ya kutoa elimu juu ya ulaji wa chakula sahihi na makundi sita ya chakula ambayo mtu anatakiwa ayapate kila siku.

Amesema ni matumaini yake mkutano huo utawawezesha kuweka mikakati zaidi kuhakikisha kilimo cha mazao ya chakula, kipatikane na kitumike kwa lishe sahihi.

Mratibu Msaidizi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), ofisi ndogo ya Zanzibar, Dorothy Temu amesema mifumo ya chakula ni miongoni mwa vipengele muhimu si kupunguza njaa tu, bali katika kuleta maendeleo.

Amesema ajenda kubwa duniani ya kuleta maendeleo inayoisha 2030 ina vipengele vitatu kuhakikisha ifikapo mwaka huo, Tanzania pia iwe imeshazifikia ikiwemo kuondoa umaskini hasa uliokithiri.

Mengine ni kuhifadhi mazingira kwani mabadiliko ya tabianchi yanachangia umaskini, amani na maendeleo kwa wote ambayo ndiyo malengo makuu ya ajenda hiyo.

“Ni vyema wadau wote kuwa na mtazamo mmoja ili kushiriki kikamilifu katika kutekeleza ajenda ya 2030 kwani ndiyo msingi wa kuleta maendeleo hapa Zanzibar,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *