Umoja wa Mataifa wahitaji dola bilioni 6 ili kupunguza janga la njaa nchini Sudan

Maafisa wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu wameomba dola bilioni 6 kwa Sudani mwaka huu kutoka kwa wafadhili ili kusaidia kupunguza kile walichokiita janga la njaa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani na kuhama kwa watu wengi kulikosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Wito huo wa Umoja wa Mataifa unawakilisha ongezeko la zaidi ya asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka jana kwa Sudani, wakati bajeti ya misaada duniani kote ikiwa katika hali ngumu, kutokana na kusitishwa kwa ufadhili uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump mwezi uliopita ambao umeathiri mipango ya kuokoa maisha ya watu duniani kote.

Umoja wa Mataifa unasema fedha hizo zinahitajika kwa sababu athari za vita vya miezi 22 kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) – ambayo tayari imewahamisha theluthi ya wakazi wake na kusababisha njaa kali kati ya takriban nusu ya wakazi wake – inaonekana kuwa mbaya zaidi.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani Cindy McCain, akizungumza kwa njia ya video kwenye chumba kilichojaa wanadiplomasia mjini Geneva, amesema: “Sudani sasa ni kitovu cha janga la njaa kubwa na kali zaidi kuwahi kutokea.”

Hakutoa takwimu maalum, lakini jumla ya wakazi wa Sudan kwa sasa ni karibu watu milioni 48. Miongoni mwa njaa za awali za kimataifa, njaa iliyoikumba Bengal mwaka 1943 iliua kati ya watu milioni 2 na 3, kulingana na makadirio mbalimbali, wakati mamilioni ya watu waliangamia kutokana na njaa nchini China katika miaka ya 1959-1961.

Hali ya njaa imeripotiwa katika angalau maeneo matano nchini Sudani, ikiwa ni pamoja na kambi za watu waliokimbia makazi yao huko Darfur, taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema, na hii inakaribia kuwa mbaya zaidi kutokana na kuendelea kwa mapigano na kuporomoka kwa huduma za msingi.

“Hili ni janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea katika kiwango chake na uzito wake na linahitaji mwitikio ambao haujawahi kutokea kwa kiwango na dhamira,” Mratibu wa Misaada ya Dharura ya Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amesema.

Moja ya kambi zilizokumbwa na njaa ilishambuliwa na RSF wiki iliyopita wakati kundi hilo la wanamgambo likijaribu kuimarisha mtego wake katika ngome yake huko Darfur.

Wakati baadhi ya mashirika ya misaada yanasema yamepokea msamaha kutoka Washington ili kutoa msaada kwa Sudani, sintofahamu inabakia juu ya kiwango cha utoaji wa misaada ya kibinadamu kusaidia wale walioathiriwa na njaa.

Mpango huo wa Umoja wa Mataifa unalenga kufikia karibu watu milioni 21 nchini humo, na kuifanya kuwa jibu kabambe zaidi la kibinadamu kufikia sasa ifikapo mwaka 2025, na linahitaji dola bilioni 4.2 – huku kiwango kitakachobaki kikienda kwa wale waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo huo.