Umoja wa Mataifa unatafuta ufadhili zaidi kwa misaada ya kibinadamu nchini Sudan

Shirika rasmi la habari la Sudan SUNA limeripoti kuwa, Umoja wa Mataifa unashirikiana na serikali ya nchi hiyo kutafuta wafadhili wa mipango yake ya misaada ya kibinadamu kwa ajaili ya mwaka ujao wa 2025.

Katika mazungumzo yake na Mona Nourel Daim, Mkuu wa Kamati ya Misaada ya Kibinadamu ya Sudan, mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Tom Fletcher amesisitizia haja ya kuongezwa juhudi za pamoja za kukabiliana na vita na migogoro inayozidi kuongezeka nchini Sudan. 

Fletcher aliwasili Port Sudan siku ya Jumamosi akiwa katika kazi yake ya kwanza ya kibinadamu tangu ateuliwe kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura huko Sudan. Alichukua jukumu hilo tarehe 18 mwezi huu wa Novemba.

Wahanga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan ni raia wa kawaida hasa wanawake na watoto

Fletcher ameitaja ziara yake hiyo kuwa ni fursa ya kutathmini hali ya kibinadamu mashinani na kusikiliza moja kwa moja malalamiko ya waoathiriwa wa vita nchini Sudan.

Sudan imetumbukia kwenye mgogoro mbaya wa ndani kati ya Wanajeshi wa Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mgogoro huo mbaya umeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 27,120 nchini Sudan.

Zaidi ya hayo, mgogoro huo umesababisha zaidi ya watu milioni 14 kuyahama makazi yao ndani na nje ya Sudan. Hayo ni kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.