Umoja wa Mataifa: Mamilioni ya watu wameathiriwa na njaa kusini mwa Afrika

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, mamilioni ya watu wako katika ukingo wa kutumbukia kwenye baa la njaa kusini mwa Afrika.

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa, mamilioni ya watu wa maeneo yote ya kusini mwa Afrika wanakabiliwa na njaa kwa sababu ya ukame ambao haujawahi kushuhudiwa na ambao unatishia kutokea maafa makubwa ya kibinadamu.

Nchi tano ambazo ni Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe, zimetangaza janga la taifa katika muda wa miezi  michache iliyopita kwa sababu ukame huo umeharibu mazao na kuangamiza mifugo.

Aidha katika taarifa yake, WFP imesema kuwa Angola na Msumbiji pia zimeathirika pakubwa na kuonya kuwa mgogoro huo unatarajiwa kuongezeka na kuendelea hadi kipindi kijacho cha mavuno yaani mwezi Machi au Aprili mwakani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mamilioni ya watu wanajongewa na janga la njaa kusini mwa Afrika

Msemaji wa WFP katika eneo la kusini mwa Afrika, Tomson Phiri, amesema  kuwa, ukame wa kihistoria umeathiri zaidi ya watu milioni 27 katika eneo hilo lote na kwamba, takriban watoto milioni 21 wana utapiamlo.

Phiri amesema, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limesambaza chakula na kusaidia mipango ya misaada lakini imepokea karibu moja ya tano tu ya dola milioni 369 inazohitaji.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imesema kuwa, makumi ya mamilioni ya watu wameathiriwa na ukame uliosababishwa na janga la El Nino katika eneo la kusini mwa Afrika na wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.