Umoja wa Mataifa: Israel ilikwamisha asilimia 85 ya majaribio ya kupelekwa misaada Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, asilimia 85 ya majaribio yake ya kuratibu misafara ya misaada na ziara za kibinadamu kaskazini mwa Gaza yalikataliwa au kuzuiwa na mamlaka ya Israel mwezi uliopita.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Miisaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa, iliwasilisha maombi 98 kwa mamlaka ya Israel ya kutaka kibali cha kuvuka kituo cha ukaguzi kwenye Bonde la Gaza, lakini ni maombi 15 pekee ndiyo yaliyokubaliwa, kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric.

Dujarric alisema OCHA “ina wasiwasi kuhusu hatima ya Wapalestina waliosalia kaskazini mwa Gaza wakati vikwazo na vizuizi vikiendelea na anatoa wito kwa haraka kwa utawala ghasibu wa Israel kufungua eneo hilo kwa operesheni za misaada ya kibinadamu kwa kiwango kinachohitajika kutokana na mahitaji makubwa”.

Aafusa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema “katika muda wa siku tatu zilizopita, timu kutoka OCHA, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu na mashirika mengine ya kibinadamu yametembelea maeneo tisa katika mji wa Gaza ili kutathmini mahitaji ya mamia ya familia zilizokimbia makazi, ambazo nyingi zinarejea kaskazini mwa Gaza. “