Marekani. Kupitia wimbo wake, ’97 Bonnie na Clyde’ kutoka katika EP yake, The Slim Shady (1998), Eminem kwa mara ya kwanza anamtaja malaika wake, Hailie Scott, hapa ndipo ulipolala moyo wake na mwanzo wa kuumbwa kwa mbingu ya ukarimu maishani mwake.
Ukitaka kujua ukali wa mbwa wa Eminem au hata kuona bastola yake, basi cheza na Hailie, binti yake wa pekee kati ya mabinti watatu aliojaliwa katika umri wake wa miaka 50.

Picha linaaza mwaka 1989 ambapo Eminem anaanzisha uhusiano na Kimberly ‘Kim’ Scott, walikutana shule, Kim alimkuta Eminem amepanda juu ya dawati akiimba wimbo wa LL Cool J, ‘I’m Bad’ na ghafla moyo wake ukanena jambo.
Uhusiano wao ukamleta duniani Hailie aliyezaliwa Desemba 25, 1995, huko Detroit, Michigan nchini Marekani, Eminem katika nyimbo kadhaa amemtaja Hailie ukiwemo, Mockingbird (2002).
Mwaka 2001 Eminem alisema kila kitu anachofanya kama kutafuta fedha ni kwa ajili ya Hailie, amemfanya kuwa makini na kupambana zaidi ya mara 10 tofauti na hapo awali.
Kwa sasa Hailie amehitimu Chuo Kikuu cha Michigan na kupata shahada ya Saikolojia kwa ufaulu wa GPA ya 3.9, alikuwa mwanafunzi bora tangu shule ya sekondari ya Chippewa Valley.

“Amenifanya nijivunie kwa hakika, hana watoto bali mpenzi tu, yupo bize na kazi zake,” alisema Eminem mwaka 2020 katika kipindi cha Hotboxin akiwa na Mike Tyson.
Hailie amekuwa akiendesha Podcast yake, Just A Little Shady, hufanya mazungumzo na rafiki na wageni, kipindi kwanza kiliruka mwaka 2022 ambapo kilimzungumzia kama mtoto wa msanii maarufu.
Lakini ni kwanini moyo wa Eminem umelala kwa Hailie licha ya awali kutajwa ana mabinti wengine wawili?, na ni kwa namna gani ametengeneza mbingu ya ukarimu?.
Wakati uhusiano wa wazazi wake unaanza mwaka 1980, Kim na pacha mwenzake, Dawn Scott walitoroka nyumbani na kuhamia kwa Eminem ambaye aliwapokea, hivyyo akawa anaishi na mpenzi wake, Kim na shemeji yake, Dawn.

Akiwa kwa Eminem, Dawn akajaliwa mtoto, Alaina Scott aliyezaliwa Februari 22, 1993, hivyo Eminem akawa anamtunza shemeji yake na mtoto wake, wakati huo Eminem na Kim bado hawajaliwa mtoto wao, Hailie.
Dawn alikumbwa na urahibu wa dawa za kulevya, hivyo Eminem akabeba jukumu la kumlea Alaina, mwanzoni mwa miaka ya 2000, aliamua kumuasili Alaina, 7, na kuwa binti yake kufuatia hali mbaya ya kiafya ya mama yake aliyekuja kufariki mwaka 2016.
Akizungumza na Rolling Stone mwaka 2020 Eminem alisema ana haki kamili ya kisheria kumlea Alaina ambaye tayari amehitimu Chuo Kikuu cha Oakland na kupata Shahada ya Sanaa katika Mawasiliano.
“Mpwa wangu amekuwa sehemu ya maisha yangu tangu kuzaliwa kwake, mimi na Kim tulikuwa naye, angeishi nasi popote tulipokuwa, ni kama binti yangu,” alisema Eminem ambaye ni mshindi wa tuzo 15 za Grammy.
Mwaka 2001 Eminem aliachana na mkewe, Kim ambaye walifunga ndoa mwaka 1999, na hapa ndipo hasa unaweza kupata picha kamili ya mbingu ya ukarimu wa Eminem.
Baada ya Kim kuachana na Eminem alianzisha uhusiano na Eric Hartter na kujaliwa mtoto mmoja, Stevie Laine Scott aliyezaliwa Aprili 16, 2002, uhusiano huku hakudumu, Kim akarejea kwa Eminem akiwa na mtoto, Mwamba akampokea kiroho safi tu!.
Mwaka 2005 Eminem akamuasili na Stevie na kuwa binti yake wa tatu, baba yake, Stevie alikuja kufariki mwaka 2019, Eminem amewatunza na kuwasomesha Alaina, 30, na Stevie, 20, tangu wakiwa wadogo hadi sasa watu wazima.
Je, ni wanaume wangapi wanaweza kuwa na moyo kama wa Eminem?, mwanaume wenye gubu, visirani na chuki kwa wapenzi wao zamani (ex) hawatoweza!, ila Eminem anamtunza mtoto wa ‘ex’ wake (Stevie) na mtoto wa dada wa ‘ex’ wake (Alaina).
Hivyo kati ya hao mabinti watatu, Hailie ndio damu pekee ya Eminem, ndipo ulipolala moyo wake, mwaka 2012 Machine Gun Kelly alitaka kucheza na moyo wa Eminem baada ya kutoa maoni Twitter kuhusu Hailie ambaye bado alikuwa chini ya miaka 18.
Miaka sita baadaye, Agosti 2018, Eminem alianzisha bifu na Kelly kwa kuachia wimbo, Not Alike, naye Kelly alijibu ‘diss track’ hiyo kwa kuachia, ‘Rap Devil’ na kuibua madai kuwa Eminem alimzuia kufika studio za Shade 45.
Eminem alitoa ‘diss’ nyingine, ‘Killshot’, wimbo uliopata ‘views’ milioni 38.1 YouTube ndani ya saa 24 na kuandika rekodi kama wimbo wa kwanza wa rap kufanya hivyo. Wiki iliyofuata, Kelly alimuomba radhi Eminem akieleza kuwa hakujua umri wa Hailie kwa wakati huo.
Na katika mahojiano yake na The Daily Mail mwaka 2018, Hailie alisema kwamba yeye na Eminem wanazungumza mara kwa mara na wako karibu sana, ila yuko karibu sana na mama yake, Kim ambaye wakati huo aliishi naye kufuatia kutengana na baba yake, pia walikuwa pamoja na ndugu zake, Stevie na Alaina.