Kikosi cha ulinzi wa anga cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimethibitisha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulio ambayo yamelenga maeneo kadhaa katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam, na kusema uchokozi huo umezimwa kwa mafanikio.
Katika taarifa kiliyotoa mapema leo, Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Iran kimesema: “licha ya maonyo yaliyotolewa na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu kwa utawala wa kihalifu na haramu wa Kizayuni wa kujiepusha na vitendo vyovyote vya chokochoko, utawala huo bandia umeshambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam asubuhi ya leo katika hatua ya kuzusha mvutano”.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, hata hivyo, Mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi umefanikiwa kuzuia na kuzima kitendo hicho cha uchokozi.
Imeelezwa kuwa mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mdogo katika baadhi ya maeneo na uchunguzi unaendelea kufanywa kubaini uzito wa tukio hilo.
Hapo awali, duru za usalama zilisema sauti kubwa zilizosikika na baadhi ya watu karibu na Tehran zilitokana na kuwashwa na kufanya kazi mitambo ya ulinzi wa anga.

Shirika rasmi la habari la Iran IRNA limenukuu duru za usalama zikieleza leo asubuhi kuwa, baadhi ya sauti zilizosikika katika mji mkuu zilisababishwa na “shughuli za kiulinzi ndani ya Tehran.”
IRNA imesema, hakuna ripoti za matukio ambayo yanahitaji kutolewa msaada na kwamba hali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini ni “ya kawaida.”
Shirika la habari la IRNA limeendelea kueleza kwamba ulinzi wa anga wa Iran “umefanikiwa kuangusha shabaha za maadui katika anga ya karibu na mkoa wa Tehran”.
Mikanda ya video iliyosambazwa mitandaoni imenasa kile kilichoonekana kama uzimaji wa shambulio lililofanywa katika mji mkuu wa Iran.
Katika upande mwingine, Shirika la Habari la Tasnim liliripoti leo asubuhi kwamba hali ilikuwa ya kawaida katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini na ule wa Mehrabad.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, hakuna shambulio lolote la kombora au athari yoyote iliyotokea kwenye vituo vya kijeshi vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) magharibi na kusini magharibi mwa Tehran.
Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Malezi amesema, skuli zote ziko wazi na shughuli za masomo zinaendelea kama kawaida.
Sambamba na hayo Tasnim imezinukuu duru za kuaminika zikieleza kwamba Iran iko tayari kujibu uchokozi wa Israel, “kama ilivyokwisha elezwa hapo awali.”
Duru hiyo imesisitiza kwa kusema: “Iran inahifadhi haki yake ya kujibu aina yoyote ya uchokozi, na hakuna shaka kuwa Israel itapata jibu mwafaka kwa hatua yoyote ambayo imechukua”…/