Ulevi ulivyosababisha meneja GPSA kusimamishwa kazi Tabora

Mwanza. Meneja wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) mkoani Tabora, Mayala Mburi ameingia matatani akidaiwa akiwa mlevi alimtukana Mkuu wa Mkoa huo, Paul Chacha na watumishi sita kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu alipotafutwa kuwapatia huduma.

Madai hayo yakitolewa, taarifa ya GPSA kupitia Kitengo cha Mawasiliano na Masoko ya Februari 20, 2025 imesema Mayala amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo. Stephen Muro, ameteuliwa kukaimu majukumu yake.

Taarifa imesema Februari 18, Chacha akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo alifanya ziara ya kushtukiza ofisi ya GPSA na kutangaza kuwa amemwelekeza Katibu Tawala Mkoa wa Tabora kumsimamisha kazi Mayala Mburi kupisha uchunguzi wa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Meneja wa Wakala wa Huduma na Ununuzi Serikalini (GPSA), Mayala Mburi wakati akijielezea kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha. Picha na mtandao

“Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) unalaani na kukemea vitendo vya aina yoyote vya utovu wa nidhamu katika utumishi ambavyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Wakala unaendelea na uchunguzi na hatimaye kuzishughulikia tuhuma hizo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Wakala umemsimamisha kazi Mayala Mburi ili kupisha uchunguzi wa suala hilo na kumteua mara moja Stephen Muro kukaimu majukumu ya nafasi hiyo na huduma zinaendelea,” imeeleza taarifa ya GPSA.

Alichosema RC Chacha

Kupitia video kwenye mitandao ya kijamii, akisimulia tukio hilo, Chacha amesema baada ya kupokea ujumbe mfupi kutoka kwa watumishi waliotukanwa alimpigia simu meneja wa GPSA lakini naye aliambulia matusi licha ya kujitambulisha jina na wadhifa wake.

“Amewasiliana yeye mwenyewe na watumishi sita kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, wanakwenda kwenye tukio kubwa Geita, akawaambia mkifika saa 2:00, saa 3:00 mtahudumiwa bila tatizo. Kumbe alikuwa hajanywa, akishakunywa huyu bwana anakuwa mtu mwingine kabisa,” amesema Chacha.

Amesema Mayala aliwasiliana na watumishi hao saa 10:00 jioni lakini wao walifika Tabora saa 3:00 usiku na kuanza kumpigia simu bila kupokewa hadi ilipofika saa 4:30 usiku ndipo ilipopokewa ikiambatana na matusi ya nguoni.

“Akawaambia ninyi ni nani mnanipigia simu usiku nipo kwenye starehe zangu? who are you by the way? aliyekupa mamlaka ya kunipigia mimi meneja wa kituo wa GPSA usiku huu niamke niache starehe zangu nije kukuhudumia, nani aliyekupa ruhusa hiyo,” amesema Chacha.

Mkuu huyo wa mkoa alisema baada ya watumishi hao kutukanwa walimtumia (RC) meseji (sms) saa 5:00 usiku naye akawapigia, ndipo wakamueleza walichokumbana nacho kisha akawaomba namba ya simu ya Mayala ili kuthibitisha kama kweli aliwatusi.

“Wakanipa namba nikampigia simu moja tu akapokea, alivyopokea akasema wewe ni nani unayenipigia usiku huu nikamwambia mimi naitwa Chacha, Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Chacha ni nani? nikamwambia mkuu wa mkoa wa Tabora. Who are you by the way mkuu wa mkoa wa Tabora unipigie simu usiku huu? Hukujua nipo kwenye starehe zangu Arusha? Nikamwambia hivi unajitambua maneno unayozungumza? Akasema najitambua na nakutambua. Tena ukome kama ulivyokoma ziwa la mama yako.

“Halafu asubuhi anakuja ananiambia nilikuwa nimelewa sana… ndivyo alivyoniambia,” amesema Chacha.

Alichosema Mayala

Akijitetea mbele ya mkuu huyo wa mkoa, Mayala amesema siku hiyo wakati anapigiwa simu alikuwa moja ya sehemu ya starehe mkoani Arusha akinywa pombe na baadhi ya watu aliowafahamu na asiowafahamu. Simu wakati inapigwa alikuwa uani, hivyo hakujua aliyeipokea.

“Kwa bahati mbaya simu nilikuwa nimeweka mziki kwa kutumia ‘bluetooth’ ya simu, kwa bahati mbaya nilikwenda uani simu yangu kumbe ilikuwa imeita kuna mteja alikuwa anataka huduma ya mafuta kwa mazingira hayo sijui aliyekuja kupokea tulikuwa unconscious anyway (hawakuwa na ufahamu),” amesema.

Amesema baada ya siku kadhaa kupita ndipo akapata taarifa kuwa kuna maneno yalizungumzwa siyo mazuri kwa mteja na kwa mkuu wa mkoa.