Ulega: Sheikh Idd amefariki kabla hajatimiza ndoto yake

Handeni. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema marehemu Sheikh Mohamed Idd amefariki dunia kabla ya kutimiza ndoto yake ya kukamilisha kitabu alichokuwa akiandika kuhusu mambo 10 muhimu ya kuzingatia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Waziri Ulega ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 31, 2025 wakati wa maziko ya Sheikh Idd yaliyofanyika katika Kijiji cha Mkata Mashariki, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Waziri Ulega alikuwa akitoa salama za rambirambi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali iko tayari kusaidia kukamilisha na kuchapisha kitabu hicho ili kuendeleza mchango wa marehemu katika kuhimiza uchaguzi huru na wa haki.

Kwa mujibu wake Novemba 25, mwaka jana na kufanya naye mazungumzo kuhusu masuala ya uchaguzi, akamweleza kwamba hata Uchaguzi Mkuu wa 2020, aliandika pia kitabu kilichoelezea mambo 10 ya msingi kuelekea uchaguzi mkuu.

“Sheikh Mohamed Idd alinifikia ili tukakidurufu kitabu kile na tutoe nakala za kutosha kabla ya uchaguzi mkuu, lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu hajafanikisha azma hiyo. Mimi nina nakala ya kitabu hicho, hivyo Mufti na viongozi wengine tuangalie namna ya kuendeleza jambo hili,” amesema Waziri Ulega.

Akizungumza katika maziko hayo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewataka Watanzania kutosikiliza maneno ya uzushi kuhusu kifo cha Sheikh Idd, huku akisisitiza kwamba mtu kukutwa na umauti ni jambo la kawaida na ni safari ambayo kila mmoja ataipitia.

Aidha, Mufti ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa kugharamia msiba huo kwa kila kitu, sambamba na rambirambi Sh50 milioni kwa familia ya marehemu.

“Kuna wanaohuzunika kama sisi… Tusitishwe na hili kwa sababu ni hali ya kawaida katika maisha; kila mmoja wetu atapitia safari hii,” amesema Mufti Zubeir.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah amesema kifo cha Sheikh Idd ni pigo kwa familia yake, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Amesema alikuwa mshauri wa masuala ya dini na mwalimu aliyewalea wanafunzi wengi wa elimu ya Kiislamu.

Mdogo wa marehemu, Zamini Juma akizungumza na Mwananchi amesema Sheikh ameacha wake wawili na watoto tisa na familia yao imepoteza mtu muhimu aliyekuwa muhimili wa ukoo wao.

“Marehemu alikuwa akituhimiza kufanya ibada na kutenda mema kila kukicha. Alikuwa akisisitiza watoto wapelekwe madrasa ili wapate elimu ya dini. Tutaendelea kumuenzi kwa kutekeleza mafundisho yake,” amesema Juma.

Kwa mujibu wa Juma, Sheikh Idd alikuwa mtoto wa nne kati ya uzao wa watoto 10 wa baba yake.

Anasema alizaliwa na kupata elimu ya dini kijijini Mkata kabla ya kujiendeleza katika Chuo cha Tamta, kilichopo mkoani Tanga.