
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema katika kuboresha sheria za ujenzi, wataingiza kipengere kitakachohitaji ili mtu apewe kibali cha kujenga, lazima awe na fundi sanifu mwenye cheti.
Amesema taaluma hiyo inapaswa kuheshimika na kupata stahiki na heshima na si kila mtu kuona anaweza kuifanya.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa saba wa siku ya mafundi sanifu uliofanyika leo Mei 22, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Ulega amesema baadhi ya watu huiona fani ya fundi sanifu kwamba yoyote anaweza kuifanya.
“Tuna mifano inapofika dakika za mwisho mambo yakaharibika, ndipo yanaanza maswali kwamba hivi hakuna wataalamu? wakati huo tayari watu wameshakufa na hasara za mali zimepatikana,” amesema.
Amesema mafundi sanifu ni kundi la lazima katika maendeleo ya miundombinu nchini ambalo linapaswa kupewa heshima.
“Tunahitaji kurasimisha sekta ya ujenzi hususan wa majengo, kwenye hotuba ya bajeti nililizungumza hili, tunahitaji kuwa na sheria ambayo itakuwa mwarobaini wa baadhi ya mambo,” amesema Ulega.
Amesema inatakiwa kuwapa kipaumbele wataalamu ambao ni mafundi sanifu huku akisema ni lazima kada hiyo iendelee kutambuliwa, kuheshimiwa na kupata haki stahiki kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Waziri Ulega ameielekeza ERB kuongeza kasi ya usajili wa mafundi sanifu ili kipengere cha kutopewa kibali cha ujenzi bila kuwa na wataalamu mwenye cheti kitakapoanza kutumika kwenye sheria, mafundi hao wawepo wa kutosha.
Amesema kwa sasa takwimu zinaonyesha Tanzania ina mafundi sanifu 3,000 waliosajiliwa, idadi aliyosema ni ndogo na kuitaka bodi kuongeza kasi ya usajili.
Waziri Ulega pia amegusia mifumo isiyoingiliana baina ya mafundi sanifu na wahandisi, akisema utakuta mhandisi analipwa mamilioni ya fedha wakati fundi sanifu anachechemea.
“Katika ufanyaji kazi ni fundi sanifu, injinia yeye utakuta anatoa maelekezo mawili matatu anakwenda kupumzika, fundi sanifu ndiye jua la kwake, vumbi la kwake halafu analipwa ujira mdogo sana,” amesema Ulega.
Amesema ni wakati sasa wa kutengeneza uwiano, vinginevyo kila mmoja (fundi sanifu) atataka atoke akatafute masilahi mazuri zaidi mahali pengine.
Msajili wa ERB, Benard Kavishe akizungumzia mkutano huo amesema unajadili mada mbalimbali ikiwamo ya changamoto, masilahi na afya ya akili.
Amesema mkutano huo umeshirikisha mafundi sanifu zaidi ya 1,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Huu ni mkutano wa saba, siku ya wasanifu ilianzishwa mwaka 2018, ikilenga kuwapa jukwaa pana kujadili kwa upekee changamoto na maendeleo ya kada hiyo.
Katika mkutano huo, mafundi sanifu wapya zaidi ya 180 waliapishwa tayari kuanza majukumu.