Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah. Ulega ameongoza Harambee maaalum ya wadau mbalimbali kuchangia Kongamano la eLearning Africa ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6 zimepatikana.
Akizungumza Aprili 16, 2025 jijini Dar es Salaam katika Harambee hiyo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania kwa mara nyingine inaingia katika historia ya kimataifa kwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo la Kimataifa ambalo lina manufaa makubwa katika taifa na kipekee katika kuimarisha sekta ya Elimu.
Amesema hakuna namna Tanzania itakwepa matumizi ya TEHAMA na teknolojia mbalimbali katika mifumo ya utoaji elimu bali ni kuhakikisha tunaenda sambamba na maendeleo hayo.
Ameongeza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kunatokana na ukweli kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amieweka nchi yetu katika ramani kupitia uimarishaji wa Diplomasia ya kimataifa, hatua hiyo imechochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.
Amewashukuru wadau wote waliojitokeza kuchangia na kuendelea kuhimiza wengine kujitokeza kuchangia na kushiriki katika hatua mbalimbali ikiwemo kuwezesha wanafunzi na wabunifu wachanga kushiriki.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukuza bunifu na teknolojia ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika elimu. Hivyo kupitia kongamano hilo wadau zaidi ya 1,500 wakiwemo Mawaziri wa Elimu kutoka Nchi zaidi ya 50 watashiriki kujadiliana mwelekeo huo.
Mkenda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Kongamano hilo kufanyika nchini ambapo taifa litanufaika kwa kiasi kukubwa kiuchumi na katika badilishana uzoefu, ujuzi, teknolojia na kupata washirika katika kuendeleza elimu kwa njia ya kidigiti.
“Mhe. Mgeni rasmi nasi hatuko nyuma tayari tuna Mkakati na miongozo ya matumizi ya teknolojia katika elimu ikiwemo matumizi ya Akili Unde, hivyo vijana, wabunifu Taasisi, Vyuo na mashirika jiandikisheni kushiriki katika kongamano, maonesho na mijadala itakayoendeshwa”
Amepongeza na kumshukuru Mgeni Rasmi kwa kuendesha zoezi hilo la uchangiaji kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha wadau kukusanya kiasi hicho cha fedha pamoja na Wizara ya Fedha mwaandaaji mwenza wa Harambee hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema tukio hilo linaonesha uwezo wa nchi katika kuandaa mikutano ya kimataifa, pamoja na kuakisi dhamira ya serikali ya kuwekeza katika elimu na teknolojia
Amesema kuwa harambee hiyo ni mwendelezo wa ushirikishaji wadau mbalimbali kuwa sehemu ya maandalizi ya Kongamano.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la 18 la Kimataifa la eLearning Africa, litakalofanyika kuanzia Mei 7 hadi 9, 2025, jijini Dar es Salaam.
The post ULEGA AONGOZA WADAU KUCHANGIA KONGAMANO LA eLEARNING AFRICA – ZAIDI YA BILIONI 1.6 YAPATIKANA appeared first on Mzalendo.