Ulega ang’aka kuchelewa miradi ya mwendo kasi, makandarasi kuchukuliwa hatua

Dar es Salaam. Mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam awamu ya nne BRT-LOT 4(1)(2) kuanzia Posta-Daraja la Kijazi hadi  Tegeta hautakamilika kwa wakati, hii ni baada ya mkandarasi kuomba mwaka mmoja wa nyongeza.

Barabara hiyo  inajengwa na makandarasi wawili mmoja ni M/s China Geo Engineering ambaye  mradi wake ni kutoka Daraja la Kijazi (Sam Nujoma) – Mwenge – Maktaba ya Taifa (Posta)  yenye urefu wa kilomita 13.5,  ambapo mwisho wa mkataba  ni Aprili mwaka huu lakini ni kilomita moja  pekee ndio imewekwa zege.

Wakati Kampuni M/s Shandog Group Co. LTD ambao wanatekeleza  mradi  kuanzia Mwenge – Tegeta (Dawasa) yenye urefu wa kilomita 15.63 mkataba wao utaisha Aprili lakini mpaka sasa wameweka zege kwenye kilomita sita pekee.

Barabara ya Ubungo hadi Kimara yenye urefu wa kilomita tano kutoka njia sita hadi njia nane ikitekelezwa na Kampuni ya China  Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) wameomba hadi Agosti mwaka huu kukamilisha mradi huo, badala ya muda wa mkataba wa kukabidhi mradi Aprili mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza na viongozi na wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kuangalia mradi huo unavyotekelezwa Dar es Salaam.

Leo Machi 5,2025 akiwa kwenye ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Ulega amewahoji makandarasi hao kwa nini miradi ambayo wanapaswa kukamilisha Aprili mwaka huu, hakuna matumaini yeyote ya kukamilika.

Mbali na maswali hayo, amehoji makandarasi hao kwa nyakati tofauti  sababu za miradi hiyo kuchelewa wakati Serikali imekamilisha malipo yote.

Kutokana na hali hiyo, Ulega ameagiza viongozi wakuu wa kampuni hizo kufika nchini kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Hata mtu asiye fundi anaona hakuna muujiza wowote kukamilisha kazi hii, hawa wanatuchezea, nimewaelekeza wawaite viongozi wao kabla ya mwezi wa tatu, nitafuata utaratibu wa kidiplomasia pia kuwaandikia barua waje hapa nchini hiki kinachofanyika hakikubaliki.”

“Hapa hakuna wafanyakazi muhimu, meneja ubora wa  mradi ndio maana kazi hii ipo nje ya muda, Serikali inakopa fedha hizi kutekeleza miradi hii kwa kazi inavyofanyika hatutawapa miradi mingine”amesema.

Muonekano wa Barabara ya Mwenge hadi Daraja la Kijazi kunakojengwa mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Waziri huyo amesema kampuni hizo zimekuwa chanzo ya foleni ya magari Dar es Salaam kutokana na kufunga baadhi ya maeneo kuchimba maeneo mengi na kusababisha magari kupita kwa shida.

Akijibu maswali ya Waziri, mwakilishi wa M/s China Geo Engineering LTD ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema kilichowakwamisha ni joto pamoja na ujenzi kufanyika eneo lenye msongamano wa  watu akiomba nyongeza ya muda.

“Tatizo ni joto na eneo ambalo tunafanya kazi katikati ya mji”amesema.

Kutokana na kauli hiyo Waziri Ulega ameng’aka akisema, “kila mahali mmechimba na hamfanyi kazi, mna mashine moja ya kuchanganya zege msituchezee mnaharibu urafiki wa Tanzania na China ambao umedumu kwa muda mrefu, napita hapa Jumamosi na Jumapili hakuna kazi inayofanyika,”amesema.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega katikati akiwa ameambatana na viongozi na wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kuangalia mradi huo unavyotekelezwa Dar es Salaam.

Waziri Ulega amesema kampuni ya M/S GEO  kulingana na mkataba wa waliousaini mwaka  2023 tayari wamelipwa Sh36 bilioni na hawana madai yeyote kwa Serikali.

Akiwa kwenye mradi wa pili wa Mwenge hadi Tegeta wa Km 15.63 , mwakilishi wa Kampuni M/S Shandog mhandisi mkazi, Sidney Bish amesema wanasukuma kazi hiyo ifanyike haraka.

“Tunafanya kazi usiku na mchana ili ikamilike mapema, ila  itatuhitaji kuongeza mwaka mmoja”amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni  Saad Mtambule amesema mwaka jana akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila walifanya ziara ya kujionea utekelezaji wa mradi huo na kukuta upo nyuma ya muda kwa asilimia 60

“Tulibaini watumishi wao ni wachache hivyo tuliwashauri wawaongeze na wafanye kazi usiku na mchana kwa sababu tunafikia kipindi cha mvua, tukawaambia ili mradi uende haraka wagawe baadhi ya kazi kwa kampuni nyingine,”amesema.

Mradi mwingine alioutembelea Ulega ni Ubungo hadi Kimara wenye urefu wa kilomita tano kutoka njia sita hadi njia nane ambao unatekelezwa na Kampuni ya China ya Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) tangu Novemba 2023.

Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo uligharimu Sh71.48 bilioni na umepangwa kukamilika kwa miezi 18.

Waziri Ulega amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anaanza kutatua kero ya foleni katika barabara hiyo.

“Maeneo mengine foleni ni kubwa sababu mkandarasi kaziba barabara yote, mkataba umekaribia kuisha na hadi sasa kazi bado, hakuna muda wa kuongeza tutachukua hatua, Wakala Barabara Tanzania (Tanroads), kaeni nileteeni mapendekezo hatua gani tuchukue kulingana na mkataba,”amesema.