‘Ukweli mchungu’! Cheki Simba na Yanga zinavyoteseka

IPO methali ya Kiswahili isemayo “Ukweli mchungu” ikiwa na maana kwamba wakati mwingine kusema ukweli huleta maumivu, huzuni au hali ngumu kwa mtu anayekubali au anayeambiwa ukweli husika.

Hata hivyo, ingawa ukweli unaweza kuumiza ni bora kuliko kudanganywa au kufichwa ukweli kwa sababu katika muda mrefu ukweli ndiyo unaoleta suluhisho la kudumu.

Kunani kwani? Licha ya kuwa Simba na Yanga zinakabana koo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku tofauti ya pointi ukiwa mdogo kati ya watani wa jadi, timu hizo zinaonekana kuwa na udhafu wa kuruhusu mabao nje ya eneo la hatari maarufu kama “penalti box”.

REKODI ZA MOTO

Kwa pamoja timu hizo za Kariakoo zimeruhusu mabao 13, Yanga saba huku Simba ikiwa sita kati ya mabao hayo, manane ambayo ni asilimia  61.5 makipa Djigui Diarra clean sheet tisa na Khomeini Abubakar (0) kwa Yanga na Moussa Camara mwenye 14 kwa Simba wamefungwa nje ya eneo la hatari.

Yanga ambao wanasuka ubingwa wa nne mfululizo, wameruhusu nusu ya mabao sawa na msimu uliopita, licha ya kwamba timu hiyo ambayo imefanya mabadiliko matatu ndani ya msimu mmoja ilianza msimu huu kwa kishindo ikishinda mechi nane mfululizo ikiwemo kuifunga Simba.

Yanga ilijikuta ikianza kuruhusu mabao katika raundi ya tisa ambapo ilifungwa 1-0 na Azam kabla ya kuruhusu matatu dhidi ya Tabora United – mechi zote hizo ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya kuhamia KMC Complex.

Katika michezo hiyo, mabao matatu moja dhidi ya Azam na mawili dhidi ya Tabora United yalifungwa ndani ya eneo la hatari, lakini moja ambalo lilikuwa la kwanza dhidi ya Nyuki wa Tabora lilikuwa nje ya eneo la hatari, Offen Chikola akimfanya kitu kibaya Diarra.

Wakati ambao Diarra hakuwa akifikiria kuwa fundi huyo wa Tabora atafanya maamuzi yale, alishangaa kuona mpira ukitinga kwenye nyavu zake, hesabu za nyota huyo ziliendana na kile ambacho mguu wake wa kushoto ulifanya.

Vipigo hivyo kwa Yanga viliotesha kibarua cha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi hivyo katika raundi ya 11 kikosi hicho kilikuwa chini ya Mjerumani, Sead Ramović na alikiongoza kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo. Katika mchezo uliofuata, Yanga ikiwa nyumbani iliruhusu mabao mawili licha ya kuibuka na ushindi wa mabao matatu.

Safari hii golini alikuwa Khomeini.

Katika mchezo huo dhidi ya Mashujaa, kipa huyo naye alijikuta akiruhusu mabao ya nje ya eneo la hatari kwa kufungwa na David Uromi na Idrisa Stambuli. Tangu hapo hakuwahi tena kupata nafasi ya kuwa golini na badala yake alikuwa akipata nafasi  Abuutwalib Mshery ambaye hakuruhusu bao hadi Diarra anapona majeraha.

Tangu hapo Yanga ilicheza michezo minne haikuruhusu bao dhidi ya Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), Fountain Gate (5-0), Kagera Sugar (4-0) na kufunga jumla ya mabao 17 kabla ya kuruhusu bao lao la nne nje ya eneo la hatari msimu huu katika ligi dhidi ya KenGold.

Pamoja na ushindi wa mabao sita, Yanga iliruhusu bao la katikati ya uwanja ambalo walifungwa na Selemani Bwenzi.

Kwa upande wa Simba mabao yote amefungwa Camara, kati ya sita ambayo Simba imeruhusu matatu ni nje ya eneo la hatari.

Tofauti na Yanga, Mnyama alianza kuruhusu mabao katika raundi ya tano dhidi ya Coastal Union wakati wakitoka sare ya mabao 2-2 baada ya kuzifunga Tabora United (3-0), Fountain Gate (4-0), Azam (2-0) na Dodoma Jiji (1-0).

Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa KMC, Simba iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 2-0, iligeuziwa kibao kwa kusawazishwa mabao yote na Hassan Abdallah na Hernest Briyock Malonga (kwa sasa upo Singida) nje ya eneo la hatari. Katika mchezo uliofuata, Camara alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuruhusu bao lingine dhidi ya Yanga, Oktoba 22, 2024.

Licha ya kwamba halikuwa bao la nje ya eneo la hatari, alifanya makosa kwa kuutema mpira wa faulo iliyochongwa na Clatous Chama huku Max Nzengeli akimalizia na kuwapa raha Wananchi kwenye uwanja wa Mkapa.

Baada ya mchezo huo, Camara alirejea kwa kishindo na kuonyesha kiwango bora katika michezo sita iliyofuata ya ligi ambapo hakuruhusu bao hata moja. Septemba 21, 2024, kipa huyo alijikuta akiruhusu mabao mawili wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Kipa huyo aliruhusu bao moja nje ya eneo la hatari ambalo alifungwa na Cleophace Mkandala na lingine la  Peter Datius lilikuwa ndani ya box. Bao lingine ambalo Camara ameruhusu ni dhidi ya Fountain Gate (1-1) ambapo alifungwa na mchezaji wake, Ladack Chasambi kwa bahati mbaya aliyekuwa na lengo la kumrudishia mpira ili kuanza upya kujenga mashambulizi yao.

NYAVU ZAO ZIMETIKISWA

Wakati Simba na Yanga zikiwa timu ambazo zimeruhusu mabao machache zaidi Ligi Kuu Bara wakifuatiwa na Azam FC ambao wameruhusu mabao tisa, Kengold ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja na Fountain Gate ndio timu ambazo zimeruhusu mabao mengi zaidi 35 kila mmoja.

Utofauti wa timu hizo, Fountain imeruhusu mabao hayo lakini wamekusanya pointi 21 ambazo zimewafanya kuwa katika nafasi ya nane, Kengold wao wametatizika kwa kushindwa kukusanya pointi za kutosha ili kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja, wapo mkiani wakiwa na pointi tisa.

MSIMAMO ULIVYO 

1. KenGold                         35

2. Fountain Gate               35

3. Kagera Sugar                 27

4. Dodoma Jiji                    24

5. Tabora United                 24

6. KMC                                  23

7. Namungo                         23

8. Tanzania Prisons            21

9. Coastal Union                  18

10. Pamba Jiji                      16

11. Mashujaa                       16

12. Singida Black Stars      15

13. JKT Tanzania                14

14. Azam FC                          9

15. Yanga                               7

16. Simba                              6