Ukraine: Uingereza yasema iko ‘tayari’ kutuma wanajeshi Ukraine ikibidi’

Uingereza imesema Jumapili Februari 16 kwamba iko tayari “kutuma wanajeshi wakenchini Ukraine ikiwa itabidi” kwa usalama wa Uingereza, pamoja na ule wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ametangaza uamuzi huo kabla ya mkutano wa viongozi wa Ulaya mjini Paris siku ya Jumatatu kujadili usalama wa bara hilo, na huku Marekani ikitaka kufanya mazungumzo moja kwa moja na Urusi ili kumaliza vita nchini Ukraine. 

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

Sweden kwa upande wake pia imetangaza kuwa inaweza ikatuma wakati wowote wanajeshi wa kulinda amani nchini Ukraine.

“Anayetaka amani hujitayarisha kwa vita”: hii inaweza kuwa kauli mbiu ya Waziri Mkuu Keir Starmer ambaye ametangaza kwamba “Uingereza iko tayari kuchukua jukumu kuu katika kuharakisha kazi ya dhamana ya usalama kwa Ukraine”, anaripoti mwandishi wetu wa London, Sidonie Gaucher.

Katika makala iliyochapishwa katika Telegraph, kiongozi wa serikali ya Uingereza anabainisha kwamba hii “pia ina maana kwamba tuko tayari na tayari kuchangia dhamana ya usalama kwa Ukraine kwa kutuma askari wetu anchini Ukraine ikiwa ni lazima.” “Sisemi hivi kwa urahisi,” ameongeza Keir Starmer, akisema anaelewa “jukumu linalokuja na uwezekano wa kuweka hatari” wanaume na wanawake wa Jeshi la Uingereza. Lakini “kusaidia kuhakikisha usalama wa Ukraine kunamaanisha kusaidia kuhakikisha usalama wa bara letu na usalama wa nchi.”

Katika taarifa yake, anathibitisha uungaji wake mkono kwa jeshi la Ukraine, haswa kwa kutoa “pauni bilioni tatu kwa mwaka hadi angalau mwaka 2030”, ambayo ni sawa na euro bilioni 3.6.

Keir Starmer amethibitisha kuwa atahudhuria mkutano wa Ulaya mjini Paris ili kukabiliana na utawala wa Marekani kuhusu suala la Ukraine. Kulingana na mshauri wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye ndiye anayeuandaa, mkutano huo unalenga “kuamua nini Wazungu wanaweza kujifanyia wenyewe kutokana na mipango ya Rais Trump kuhusu suala la Ukraine.”

Kulingana na Élysée, “wakuu wa serikali ya Ujerumani, Uingereza, Italia, Poland, Uhispania, Uholanzi na Denmark, na vile vile Rais wa Baraza la Ulaya, Rais wa Tume ya Ulaya na Katibu Mkuu wa NATO” watashiriki katika “mkutano hu usio rasmi” leo alasiri.

Saa chache baada ya uamuzi wa London, Sweden imetangaza kuwa haiondoi hioja ya kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini Ukraine. “Lazima kwanza tujadili sasa amani ya haki na ya kudumu ambayo inaheshimu sheria za kimataifa (…) Tunapokuwa na amani hii iliyoanzishwa, itabidi idumishwe na kwa hili, serikali yetu haiondoi chochote,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Maria Malmer ameiambia redio ya umma ya Sveriges Radio.

Mipango ya Marekani inatia wasiwasi nchi za Ulaya

Kwa sababu Donald Trump amezindua mipango inayowatia wasiwasi Wazungu. Rais wa Marekani, ambaye ameanza tena mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ametoa matangazo mengi kwamba anataka kuanza mchakato wa amani.

Alisema wiki hii kwamba atakutana na mwenzake wa Urusi nchini Saudi Arabia ili kuanza mazungumzo kuhusu Ukraine, ambapo vita vilivyochochewa na uvamizi wa Urusi vitaingia mwaka wake wa nne Februari 24. Alipoulizwa Jumapili, Februari 16, kuhusu tarehe ya mkutano huu, Bw. Trump alijibu: “Hakuna tarehe iliyowekwa, lakini inaweza kuwa hivi karibuni.”

Katika muktadha huu, Keir Starmer pia amesema kwamba atakutana “katika siku zijazo” na Rais wa Marekani Donald Trump. Uingereza ina “jukumu la kipekee” la kutekeleza katika kuhakikisha kuwa Ulaya na Marekani zinashirikiana kwa karibu, kulingana na Waziri Mkuu wa Uingereza.

Rais wa Ukraine kwa upande wake amesema hana mpango wa kukutana na maafisa wa Urusi au Marekani kwa sasa. Volodymyr Zelensky alitangaza Jumapili jioni kwamba aliwasili katika Falme za Kiarabu kwa ziara ya “kibinadamu”. Atasafiri kwenda Saudi Arabia siku ya Jumatano, Februari 19, siku moja baada ya mazungumzo ya Urusi na Marekani mjini Riyadh, msemaji wake ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu.