Ukraine: Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Urusi yamethibitishwa

Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Ukraine na Urusi yanakaribia, lakini bado kuna safari ndefu. Wapatanishi wa Marekani, ambao wanatarajiwa kuwasilisha pendekezo la Donald Trump la kusitisha mapigano kwa siku 30 nchini Ukraine kwa Kremlin, wako njiani kuelekea Urusi, Kremlin imetangaza leo Alhamisi, Machi 13.

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

“Wapatanishi wanawasili kwa ndege na mawasiliano yamepangwa,” msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov amesema wakati wa mkutano wake wa kila siku, ambao shirika la habari la AFP limehudhuria. Ameongeza kuwa Mshauri wa Usalama wa taifa wa Marekani Mike Waltz na mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Vladimir Putin, Yuri Ushakov, walipigiana simu siku ya Jumatano.

Donald Trump alihakikisha kwamba amepokea “ujumbe chanya” kutoka Moscow ili kukomesha “umwagaji damu huu wa kutisha.”

Pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 30, baada ya zaidi ya miaka mitatu ya mzozo, lilikubaliwa na Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky na linawekwa kuwa kiini cha majadiliano kati ya wakuu wa diplomasia wa nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda za G7, ambao wanakutana tangu Alhamisi asubuhi huko Charlevoix, nchini Canada.

Mashambulizi na majibu

Lakini wakati haya yote yanafanyika, nchi hizo mbili zinaendelea kushambuliana. Urusi imedai kuurejesha mji wa Sudja, mji mkuu wa Ukraine uliotekwa katika eneo la Kursk, siku ya Alhamisi, katika hatua ambayo ingeashiria kikwazo kikubwa kwa mashambulizi ya Kiev. Vijiji viwili vya karibu, Melovoi na Podol, pia vimetekwa.

Rais wa Urusi, akiwa amevalia sare za kijeshi, alitembelea wanajeshi wake karibu na Kursk siku ya Jumatano na kuamuru jeshi lake “kukomboa kabisa” eneo la mpaka lililochukuliwa na vikosi vya Ukraine. Mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kherson Roman Mrochko amesema leo Alhamisi kwamba mtu mmoja aliuawa katika shambulio la anga la Urusi lililopiga mji huo kusini mwa Ukraine.

Wakati huo huo, usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Ukraine, kubwa zaidi tangu shambulio hilo dhidi ya Ukraine, lililenga mkoa wa Moscow haswa, na kuua watu wasiopungua watatu. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema leo Alhamisi kuwa ilitungua ndege zisizo na rubani 77 za Ukraine usiku kucha katika maeneo mbalimbali ya Urusi, zikiwemo 30 kwenye mpaka wa Bryansk, kwenye mpaka wa Ukraine, na 25 juu ya anga ya Kaluga.

“Shinikizo la juu”

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema askari wa Urusi “wanajaribu kwa uwazi kuweka shinikizo kubwa” kwa kikosi cha Ukraine kilichoingia katika eneo hilo katika majira ya joto ya mwaka 2024. Hivyo amesema kuwa watu wake wameondoka kwenye maeneo haya ambapo jeshi la Urusi limedai kupata mafanikio ya haraka katika siku za hivi karibuni.

“Mazungumzo ya simu katika ngazi ya juu” kati ya Trump na Putin yanawezekana kwa “muda mfupi,” msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov amesema.

Mapema mwezi huu, hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema kusitisha mapigano kwa muda “hakukubaliki.”

Kwa kusubiri jibu la Urusi

Pendekezo la kusitisha mapigano lilikuja baada ya mazungumzo siku ya Jumanne nchini Saudi Arabia kati ya maafisa wa Ukraine na Marekani. Mkutano huo ulimaliza kipindi cha mvutano kati ya Kyiv na Washington kufuatia mkutano mkali kati ya Donald Trump na Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House.

Rais Zelensky pia amehimiza Urusi kuamua juu ya pendekezo la Marekani, huku akihakikishia kwamba kwa vyovyote vile “hamuamini”. Ametoa wito kwa Marekani kuchukua hatua “kali” katika suala la vikwazo na msaada kwa Ukraine iwapo Urusi itakataa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema “anasubiri kwa hamu” majibu ya Urusi “kujua kama wako tayari” kukubali kusitishwa kwa mapigano “bila masharti.”

“Ikiwa jibu ni ‘ndiyo,’ basi tunajua tumepata maendeleo ya kweli na kuna nafasi ya kweli ya amani. “Ikiwa jibu lao ni ‘hapana,’ itakuwa ni bahati mbaya sana na itaweka wazi nia yao,” alieleza jana Jumatano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *