Dodoma. Wabunge wameibua mjadala kuhusu mabando wanayonunua kwenye kampuni za simu kwisha kabla ya kutumika, wakieleza hiyo ni dalili ya wizi.
Pia wamezungumzia matumizi ya akili mnemba (AI), wizi wa kutumia mitandao na hisa zilizowekezwa katika kampuni ya Vodacom.
Kwa nyakati tofauti wameibua hoja hizo bungeni leo Ijumaa Mei 16, 2025 walipochangia mjadala kuhusu hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Waziri wa wizara hiyo, Jerry Silaa ameliomba Bunge liliidhinishe Sh291.53 bilioni kati ya hizo Sh277.04 bilioni zikipelekwa katika miradi ya maendeleo.
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul ameelezwa kuchangazwa kuona wizi wa mtadaoni ukishindwa kudhibitiwa, akisema wizara hiyo inaweza kufanya hivyo iwapo itaamua.
Pia amezungumzia alichokiita wizi kwenye mabando ya simu akitoa mfano kuna watu ambao hununua na hata akizima simu anapowasha anakuta ujumbe kuwa bando lake limekwisha akieleza ni wizi unaoweza kuzuilika.
“Huu ni wizi, inakuwaje mtu anatoa fedha zake kununua bando halafu anakuwa amezima simu lakini baada ya muda anaambiwa kuwa kifurushi chake kimekwisha, siyo sawa lazima tuliangalie hili,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba pia amezungumzia wizi wa mitandao akihoji Serikali inakwama wapi kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya mawasiliano watu ambao wanajihusisha na wizi huo.
Amesema majina ya viongozi yamekuwa yakitumika katika wizi huo lakini wizara na vitengo vyake imeshindwa kuwasaidia kudhibiti jambo hilo.
Ametaja aina nyingine aliyoiita wizi kwenye mitandao ya simu akisema mtu akituma fedha kimakosa akaomba zirudishwe, kiasi alichotuma hurudishwa lakini gharama hazirudi.
“Kama hamtaangalia hili linakwenda kuwaumiza sana watu hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, ni tatizo tena kubwa,” amesema.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi amekiri kuwa wizi wa mitandao ni janga kubwa lakini linalotokana na matumizi yasiyo sahihi ya ukuaji wa teknolojia.
Mahundi amesema wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu, akitoa wito kwa wananchi kuwa makini.
Hisa Vodacom
Makamba amezungumzia hisa za Vodacom akisema aliyenunua kwa Sh10 milioni, hivi sasa anauza kwa Sh8 milioni lakini hakuna anayenunua.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu pia amezungumzia hisa hizo akisema nia ya ununuzi ilikuwa njema, lakini kinyume chake imekuwa ni kilio na msiba kwa wananchi hasa wawekezaji ambao baadhi walikopa fedha ili kuzinunua kutokana na gawio.
Ametoa mfano mwaka 2017 kuna watu walinunua hisa hizo lakini gawio walilopewa mwaka 2024 lilikuwa maumivu yasiyoelezeka.
Kwa mujibu wa Kingu, wastani wa hisa ambazo watu wamepata kwa kipindi chote cha uwekezaji ni Sh245 ambayo ni sawa na Sh35 tu kwa kila mwaka ambayo amesema hakuna uwekezaji mbovu kama huo.
Mbunge wa Nyamagana, Staslaus Mabula amesema kuna watu katika jimbo lake wamechukuliwa nyumba zao kutokana na madeni waliyokopa benki na taasisi za fedha ili wawekeze lakini leo hii wanakufa maskini.
“Lakini kibaya zaidi hebu fikiria mtu aliwekeza Sh60 milioni mwaka 2017 halafu mwaka jana (2024) mtu anakuja kupata gawio la Sh700,000 kama si uuaji ni nini, tunaitaka Serikali iingilie kati ili ama kuifuta sheria hii au Watanzania warudishiwe fedha zao,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanaisha Ulenge katika hilo amesema anachohitaji ni kuona namna gani anaweza kupata fedha zake alizowekeza katika kampuni hiyo.
Majibu ya Waziri, Vodacom
Akijibu hoja za wabunge, Waziri Silaa amewaomba wabunge wampe muda ili azungumze na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) washauriane.
“…nimepokea, lakini hili la hisa naomba mtupe nafasi ili nikae na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tujadiliane kisha tutakuwa na cha kusema kwa wabunge,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Philip Besiimire amesema gawio limekuwa likitolewa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Amesema hutolewa kutoka faida iliyopatikana na baada ya kupitishwa na mkutano mkuu. Amesema hata mwaka huu wanatarajia kutoa gawio.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 leo Mei 16, 2025.
“Faida kwa hisa imekuwa ikiongezeka kila mwaka na mwaka huu kutokana na ufanisi mzuri tutarajie ongezeko hilo pia,” amesema kwenye mkutano wa kampuni hiyo uliofanyika leo Mei 16 kutangaza hesabu za awali za mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2025.
Amesema alikuwa bungeni amesikia hoja za wabunge, hivyo watafanyia kazi baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wanahisa kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuongeza uelewa.
Amesema kama kuna ambao hawajapata gawio lao itakuwa ni masuala ya kimenejimenti, hivyo watalifuatilia kwa karibu na washirika wao kuhakikisha kila mtu anapata gawio lake.
Mkurugenzi Mtendaji wa idara ya fedha katika kampuni hiyo, Hilda Bujiku amesema gawio limekuwa likitolewa pengine thamani ndiyo imekuwa hairidhishi wawekezaji lakini kampuni hiyo inaendelea kufanya kazi kuhakikisha wawekezaji wanafurahia uwekezaji wao.
“Thamani nayo inaweza kuonekana ndogo kwa kuwa tunalinganishwa na wengine tulionao sokoni lakini waliopo si watu wa sekta yetu, sekta yetu tuko pekee yetu hivyo tunakosa ulinganisho sahihi,” amesema.