
KATIKA harakati za kuhakikisha nidhamu inaimarika ndani ya kikosi, uongozi wa Singida Black Stars umeweka utaratibu wa adhabu mbalimbali kwa wachezaji wanaokiuka misingi na taratibu za timu hiyo.
Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Jonathan Kasano amefichua kuwa kila mchezaji atakayekiuka taratibu zilizowekwa ikiwamo kuchelewa mazoezini au makubaliano atakatwa Dola 200 (takribani Sh528,491) kutoka kwenye mshahara.
“Tumeamua kuwa na mfumo wa adhabu kwa ajili ya nidhamu. Mchezaji ambaye atachelewa kwenye mazoezi, mikutano ya timu au kuvunja masharti mengine tuliyokubaliana atakatwa Dola 200 moja kwa moja,” alisema Kasano.
Mtendaji huyo aliongeza kwamba uamuzi huo sio wa kuwaumiza wachezaji, bali ni njia ya kuhakikisha nidhamu inazingatiwa ili timu iweze kufanikiwa.
“Soka la kisasa linahitaji nidhamu. Huwezi kuwa na timu bora kama wachezaji hawaheshimu muda na maelekezo ya benchi la ufundi,” alisisitiza.
Mfumo huo wa adhabu sio wa kwanza nchini.
Timu kama Simba, Yanga na Azam FC pia zina utaratibu wa kuwaadhibu wachezaji wanaochelewa mazoezini au kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa.
Kwa mfano Nasreddine Nabi wakati akiwa kocha wa Yanga aliwahi kuwafukuza baadhi ya mastaa wa timu hiyo na waliokosa mechi baada ya kuchelewa kuripoti kambini.
Kasano amesisitiza kuwa adhabu hizo zinaleta uwajibikaji ndani ya Singida Black Stars.
“Mchezaji anapojua kuwa kuchelewa kunamaanisha atakatwa mshahara wake, atajitahidi kuheshimu ratiba. Tuna malengo makubwa na haya ni baadhi ya mambo tunayofanya ili kuyafanikisha,” alisema.
Hata hivyo, tangu kuwekwa kwa adhabu hiyo hakuna mchezaji wa Singida Black Stars ambaye amekumbwa na rungu hilo.
Mmoja wa wachezaji ambaye hakutaka jina lake litajwe alizungumzia adhabu hiyo kwa kusema: “Tunajua nidhamu ni muhimu, lakini Dola 200 ni nyingi sana. Ingekuwa vizuri kama wangepunguza kiasi hicho.”
Kwa upande wa benchi la ufundi la timu hiyo, linaunga mkono hatua hiyo likisema itasaidia kuimarisha nidhamu na kushinikiza wachezaji kuwajibika zaidi.