Ukistaajabu ya Rita wa Diamond utayaona ya Rita wa Bob Marley

Dar es Salaam. Katitati ya wiki iliyopita hali ya hewa ilichafuka mitandaoni baada ya kuvuja kwa video zikimuonyesha mrembo mmoja anayeitwa Rita Norbeth akiwa na nyota wa muziki, Diamond Platinum, kwenye mahaba makubwa.

Baada ya kuvuja kwa video hizo, haraka haraka Diamond akaibuka na ‘kuzikana’ akisema yeye na mrembo huyo walishaachana tangu mwaka 2023. Diamond alikuwa anapambana kulinda heshima yake ili video zile zisimharibie mambo kwa mpenzi wake, Zuchu.

Lakini bibie Rita Norbeth akaibuka na kusema anachosema Diamond si kweli, kwani 2023 haukuwa wa kuachana, bali kubainika kwa mahusiano yao kwa Zuchu, lakini waliendelea kuwa wapenzi hadi 2024.

Rita hakuishia hapo akaenda mbali na kulalamika kwamba alinyanyaswa kihisia na Diamond walipokuwa Afrika Kusini.

Akasema kwamba, Diamond alilala na mwanamke mwingine wa kuitwa Fantana, kwenye chumba kingine akimuacha yeye peke yake kwa kuwa alikuwa hedhi. Malalamiko hayo ya mrembo huyo ndio yanayonifanya niukumbuke mkasa wa mwanamke mwingine mwenye jina la RITA, aliyekuwa mke wa mfalme wa muziki wa reggae, hayati Bob Marley. Jina lake halisi ni Rita Anderson, lakini baada ya kufunga ndoa na Bob Marley akaitwa Rita Marley.

Rita ni mmoja wa wanawake watatu wa kundi la I Threes ambao waliungana na Bob Marley na kuunda kundi la Bob Marley & The Wailers 1973 baada ya Bob Marley kuhitilafiana na marafiki zake, Peter Tosh na Bunny Wailer. Wenzake na Rita walikuwa Marcia Griffiths na Judy Mowatt. Hao ndio wale wanawake watatu ambao huitikia nyimbo za Bob Marley.

Hata wimbo wa Three Little Birds, ambao Klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi inautumia kama wimbo wake rasmi, Bob Marley aliwatungia wanawake hawa, kwamba hao ndio three little birds yaani ndege wadogo watatu.

Bob Marley na Rita walifunga ndoa 1966, lakini maisha ya umaarufu yaliwapitisha kwenye njia mbaya na ya aibu. Kwa mujibu wa Rita Marley ambaye pia alikuwa mwimbaji wa bendi ya Bob Marley & The Wailers, ilifikia wakati mumewe alikuwa akimtuma amletee mwanamke alale naye wakiwa kwenye ziara za muziki.

Kwanza Bob Marley alimpata mrembo mwingine wa Jamaica, Cindy Shakespeare, aliyeshinda mashindano ya urembo ya dunia (Miss World 1976). Huyu ndiye mama wa Damian Marley, mmoja wa watoto maarufu wa Bob Marley aliyetamba sana na wimbo wa Beautiful alioimba na Bobby Brown.

Hata hivyo, Bob Marley hakuridhika na mwanamke huyo, bado akawa na wengine wengi wakiweko wale ambao alikuwa akimtuma Rita amletee. Maisha hayo yakamchosha Rita na yeye akaamua kutafuta mtu wa kumpumzikia, akampata Owen ‘Ital Tacky’ Stewart, mwanasoka maarufu wa wakati huo. Akazaa naye mtoto mmoja wa kike aliyeitwa Stephanie, ambaye Bob Marley alimchukua na kuwa mwanawe kwa sababu hakuwahi kumpa talaka Rita.

Stephanie Marley ni mmoja wa watoto rasmi wa Bob Marley waliopo kwenye orodha inayotambuliwa kisheria na kuhusika na mirathi kama watoto wengine. Na hii ndio aibu niliyoizugumzia hapo awali. Yaani staa mkubwa kama Bob Marley analazimika kuchukua mtoto ambaye si wake kwa sababu tu ya kulipa gharama za ‘ukora’ wake.

Bob Marley ni shujaa wa sanaa na harakati za haki za bibadamu, lakini maisha yake ya mahusiano siyo ya kuigwa hata kidogo. Katika kitabu chake cha kumbukumbu ya maisha yake na Bob Marley alichokiita No Woman No Cry: My Life with Bob Marley, Rita anasema alipitia changamoto nyingi na Bob Marley.

Wakikutana studio, yeye akiwa na miaka 18 na mwaka mmoja baadaye wakafunga ndoa wakiwa hawana chochote, sio umaarufu wala hela. Wakiwa pamoja wakafanikiwa kuwa maarufu na matajiri wakubwa. Umaarufu na utajiri huo ukawa mtihani mkubwa kwao na kuwapitisha kwenye njia ya majaribu makubwa.

Lakini, licha ya misukosuko yote hiyo wawili hao waliendelea kuwa mke na mume hadi kifo cha Bob Marley 1981. Kwa lugha ya kimjini ya sasa, Rita Marley alikuwa king’ang’a hasa licha ya kuchapwa matukio yaliyomtingisha hadi kuzaa nje ya ndoa.

Rita wa Bob Marley alishindwa kuvumilia kuendelea kulala peke yake, huku akishuhudia mumewe wa ndoa akiwa na mwanamke mwingine aliyemleta yeye mwenyewe. Na mimi naamini kabisa kwamba hata RITA WA DIAMOND PLATINUMZ naye hawezi kuvumilia hilo. Ni lazima tu alimtafuta mtu wa kumpuzikia, ili kulipa kisasi katika kutafuta unafuu wa nafsi.

Na baada ya kuona unafuu hauji ndio maana akaamua kuachia video hizo, japo mwenyewe anasema hakutoa yeye. Vyovyote itakavyokuwa, kwa mara nyingine jina la Rita limekuwa mhanga wa msanii mkubwa anayeishi kwenye bahari ya pesa na umaarufu, lakini mwenye udhaifu mkubwa wa wanawake. Na bila shaka yale ya Afrika Kusini ni machache, yawezekana kuna mengi hatuyajui kutoka kwa Rita Norbeth, aliyokutana nayo kutoka kwa Diamond.

Ukiacha ya Rita hao wawili, maisha ya wanaume wao nao ni kama yanafanana. Bob Marley ni mwanamuziki aliyezaliwa na kulelewa na mama yake. Baba yake, Captain Norval Sinclair Marley, alifariki dunia wakati yeye akiwa na miaka 12 lakini hakuwahi kumuona.

Na haya ndo maisha ya Diamond. Alizaliwa na kulelewa na mama na hadi leo ni mtoto wa mama. Baba yake mzazi alikuja kumfahamu ukubwani, na haikuchukua muda akafariki dunia. Akabaki analelewa na mama hadi akatoboa. Na hata mitaa waliyokulia. Bob Marley alikulia Trench Town, mitaa ya watu masikini alikokua akiishi na mama yake.

Diamond amekulia Tandale, mitaa ya watu masikini alikokua akiishi na mama yake. Mgongano huo wa matukio, na kuwa wanawake wenye jina lilalofanana ni ajabu, lakini kuwapiga wanawake hao matukio yanayofanana ndiyo ajabu zaidi.

Rita wa Bob Marley aliandika kitabu kilichoitwa No Woman No Cry…nadhani Rita wa Diamond naye asiishie kutuandikia kwenye Instagram aje na kitabu ili tuyajue tusiyoyajua katika mahusiano yao.