Ukishangaa ya Beyonce, utaona ya Harmonize

Dar es Salaam, Licha ya Harmonize kutajwa kuwania vipengele saba Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023, huenda akakutana na yale ya Beyonce Knowles katika tuzo za Grammy tangu aanze kuwania miaka ya 1990 na kundi lake la Destiny’s Child.

Beyonce ameshinda tuzo 32 za Grammy na ndiye kinara duniani hadi sasa lakini hajawahi kushinda kipengele cha Albamu Bora kwa miaka yote aliyowania kati ya albamu zake nane alizotoa.  

Tangu kuachia albamu ya kwanza kama solo, Dangerously in Love (2003) kufuatia kusambaratika kwa Destiny’s Child, Beyonce amewania kipengele cha Albamu Bora tuzo za Grammy kwa mara nne bila ushindi wowote.

Ikumbukwe mwaka 2010 aliwania Grammy kupitia albamu yake, I Am … Sasha Fierce (2008), kisha 2015 kupitia Beyonce (2013), 2017 kupitia Lemonade (2016) na 2023 kupitia Renaissance (2022).

Jinsi ilivyokuwa vigumu kwa Beyonce kushinda tuzo ya Albamu Bora Grammy, ndivyo ilivyo kwa Harmonize upande wa TMA akiwa tayari amewania mara mbili bila ushindi na sasa anaenda kujaribu mara ya tatu.

TMA 2023 Harmonize anawania Msanii Bora wa Kiume, Albamu Bora (Visit Bongo), Wimbo Bora (Single Again), Mtumbuizaji Bora, Msanii Bora wa Kiume Bongo Fleva, Video Bora (Single Again Remix ft. Ruger) na Wimbo Bora wa Bongo  Fleva (Single Again).

Utakumbuka tayari ameshinda tuzo nne za TMA, msimu wa 2021 alishinda kama Mtumbuizaji Bora wa Kiume, Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Attitude ft. Awilo Longomba & H. Baba) na Msanii Bora wa Kiume.

Na msimu wa 2022 alishinda tuzo moja ya Msanii Bora wa Kiume Bongo Fleva, kwa kifupi ameshinda vipengele vingi vikubwa vya TMA ila kile cha Albamu Bora ndicho kinamtoa jasho kama Beyonce kule Grammy, tuzo zilizoazishwa miaka 65 iliyopita.

Albamu yake ya pili, ‘High School’ iliwania TMA 2021 ikakosa, ilichuana na albamu nyingine kama ‘Ona’ ya Marco Chali, ‘Live At Sauti za Busara’ ya Wakazi, ‘Air Weusi’ ya Weusi na Only One King ya Alikiba iliyoibuka na ushindi.

Akarejea tena TMA 2022 na albamu yake ya ‘Made For Us’ ila akaangukia pua tena, awamu hii ilichuana na albamu kama ‘The Kid You Know’ ya Marioo, ‘Street Ties’ ya Conboi, ‘Romantic’ ya Kusah na ‘Love Sounds Different’ ya Barnaba iliyoshinda.

Na sasa TMA 2023 Harmonize amerusha karata yake tena kupitia albamu ‘Visit Bongo’ ambayo inashindama na nyingine nne ambazo ni ‘5’ ya Abigail Chams, ‘Swahili Kid’ ya D Voice, ‘Most People Want This’ ya Navy Kenzo na ‘Flowers III’ ya Rayvanny.

Albamu ya Visit Bongo (2023) ndiyo ina wimbo wa ‘Single Again’ ambao umetajwa katika vipengele vitatu, sasa shauku ya mashabiki wengi ni kuona kama hilo litambeba awamu hii katika kipengele cha Albamu Bora au ndiyo itakuwa yale yale ya Beyonce?.

Ikumbukwe Harmonize mwenye albamu tano na EP moja, ndiye mwanamuziki wa kwanza wa Bongo Fleva kutajwa kuwania Albamu Bora TMA kwa mara tatu mfululizo ikiwa ni msimu wa 2021, 2022 na 2023.

Eneo lingine analotolea macho Harmonize ambaye anawania vipengele saba TMA 2023, ni kuona kama itaifikia na kuivunja rekodi aliyoweka Zuchu msimu uliopita ambapo alishinda tuzo tano kwa usiku mmoja.  

Utakumbuka Zuchu alishinda TMA 2022 kama Msanii Bora wa Kike, Video Bora (Mwambieni), Msanii Bora wa Kike Bongo Fleva, Wimbo Bora wa Bongofleva (Kwikwi) na Msanii Bora wa Kike Chaguo la Watu Kidijitali.

Kwa matokeo hayo, Zuchu aliifikia rekodi ya Alikiba katika TMA 2021 aliposhinda tuzo tano kama Mtumbuizaji Bora, Albamu Bora (Only One King), Msanii Bora wa Kiume Chaguo la Watu Kidijitali, Msanii Bora Afrika Mashariki na Video Bora (Salute ft. Rudeboy).

Tuzo za TMA ambazo zilianzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa msimu wa 2023 zinatarajiwa kutolewa hapo Septemba 29 mwaka huu ikiwa ni siku moja baada ya kufungwa kwa zoezi la upigaji kura.