Ukipigwa umekwisha mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu Bara zimeshika kasi na kufikia patamu. Licha ya kwamba hadi sasa ubingwa huo kuwa wazi kwa timu tano, lakini Simba na Yanga wakionekana na nafasi nzuri.

Simba ndio inaongoza msimamo ikiwa na pointi 47 moja zaidi na ilizonazo Yanga ambao ni watetezi, huku Azam ikiwa ya tatu ikiwa na pointi 39 ikifuatiwa na Singida Black Stars yenye 34 na Tabora United ikifunga Tano Bora ikiwa na pointi 31 kila timu ikisaliwa na mechi 12.

Utamu zaidi ni kwamba mechi zilizosalia kwa kila timu, baadhi zitazikutanisha zenyewe kwa zenyewe, ikiwa na maana yeyote atakayekubali kupoteza itakula kwake mazima kabla ya msimu kufungwa Mei 28.

Kama hujui, kuna kitu Simba na Yanga wanakabiliana nacho katika safari ya kuwania ubingwa msimu huu huku wakiwa na vikwazo vinne mbele yao. Vikwazo hivyo wanahitaji kuvivuka kabla ya Machi 8 wababe hao kukutana katika mchezo unaoweza kutoa picha halisi, huku kwa sasa kila timu ikiwa imecheza mechi 18.

Yanga chini ya Kocha Miloud Hamdi inapiga hesabu nzito za kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Upande wa Simba inayonolewa na Kocha Fadlu Davids, baada ya kulikosa taji hilo misimu mitatu mfululizo, safari hii inalitolea macho ikiwa na mabadiliko makubwa ndani ya kikosi.

Simba iliyobeba taji la Ligi Kuu Bara mara ya mwisho 2020-2021 chini ya Kocha Didier Gomes, imekuwa ikifukuzia ubingwa bila mafanikio, huku ikibadili benchi la ufundi kwa kuleta makocha kutoka nje ikianza na Pablo Franco, Zoran Maki, Roberto Oliveira ‘Robertinho na Abdelhak Benchikha ambao wameshindwa kulibeba.

Yanga ambayo msimu huu inataka kutetea tena ubingwa imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi ikimtoa Miguel Gamondi akaja Sead Ramovic na sasa yupo Hamdi kumalizia msimu huu.

VIGINGI VILIVYO

Kabla ya Machi 8 mwaka huu, ratiba inaonyesha  Simba na Yanga kila moja itakuwa na mechi nne za ligi ambazo zimekaa kimtego. Hata hivyo ajali iliyoihusu Dodoma Jiji imefanya pambano baina yao na Simba kuondolewa na hivyo Simba kusaliwa na michezo mitatu kabla ya kuvaana na Yanga.

Pia katika mechi hizo kila moja itacheza mbili nje ya Dar na Yanga itakiwa na michezo miwili nyumbani wakati Simba kwa kuahirishwa mchezo wa Dodoma imesaliwa na mmoja  nyumbani kitu ambacho umakini unahitajika ili kubaki kwenye mstari kabla ya mechi ya hukumu baina yao.

Rekodi zinaonyesha Simba na Yanga katika mechi ilizocheza nje ya Dar hakuna aliyepoteza, hivyo inaonekana zimekuwa makini kukabiliana na wapinzani wao sambamba na wale wanaokuja ili wasitibue mipango yao.

Kama mambo yatakwenda hivi kupishana pointi moja hadi Machi 8 zitakapokutana inaweza kuwa mechi ngumu zaidi kama ile ya duru la kwanza Yanga iliposhinda 1-0 lililotokana na beki wa Simba, Kelvin Kijiri kujifunga dakika ya 86.

Vinara hao katika mechi zao nne zijazo watakabiliana na timu ambazo duru la kwanza ilikusanya pointi ilipokutana nazo ambapo tatu ilishinda na moja sare.

Kwa sasa haitacheza tena mechi ya Februari 15, 2025 dhidi ya Dodoma Jiji kutokana kupata ajali walipokuwa wakitoka Lindi kuja Dar walikokwenda kucheza dhidi ya Namungo. Kuahirishwa kwa mchezo huo kunatoa nafasi kwa Simba kupata muda mwingi wa kujiandaa kabla ya mchezo ujao utakaopigwa ugenini dhidi ya Namungo Februari 19 katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi baada ya duru la kwanza Simba nyumbani kushinda 3-0.

Rekodi zinaonyesha Simba katika mechi tano nyumbani kwa Namungo imeshinda moja huku nne ikitoka sare, haijapoteza. Namungo rekodi za nyumbani msimu huu katika mechi nane imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza nne hali inayoonyesha haina matokeo mazuri wakati Simba tisa za ugenini imeshinda nane na sare moja. Februari 24, 2025, Simba itaikaribisha Azam, timu ambayo nayo inafukuzia nafasi za juu ambapo ni ya tatu na pointi 39, imeachwa pointi nane na vinara Simba.

Ni mchezo ambao Azam inayofundishwa na Rachid Taoussi itahitaji kulipa kisasi baada ya duru la kwanza ikiwa mwenyeji kupigwa 2-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Kigingi cha nne kwa Simba kitakuwepo Machi 1, 2025 itakapokwenda Arusha kucheza na Coastal Union inayotumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kipa wa Simba, Moussa Camara ana kumbukumbu mbaya alipokutana na Coastal Union duru la kwanza kwani alifungwa mabao mawili ya mbali katika sare ya 2-2 iliyomtibulia kwani aliruhusu nyavu kutikiswa kwa mara ya kwanza baada ya mechi nne mfululizo kuondoka na clean sheet.

Suluhu dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliopita kwa kiasi fulani imewatibulia mipango ya kuendelea kukaa kileleni na kuiacha Simba kurudi eneo ililokaa kwa muda mrefu. Muda wa kurekebisha walipokosea ni huu kwani mchezo unaofuata ni kesho watakapokuwa wageni wa KMC, mechi ikipigwa Uwanja wa KMC Complex.

Bao la Maxi Nzengeli katika duru la kwanza lilitosha kuipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC, huku mchezo wa kesho unaweza kuwa tofauti baada ya KMC kuishangaza Singida Black Stars kwa kuifunga.

Baada ya mchezo huo, Februari 17 Yanga itaikaribisha Singida Black Stars ambayo nayo imefanya maboresho makubwa ya kikosi chake. Duru la kwanza Yanga ilishinda 1-0 ikiwa ugenini, safari hii ipo nyumbani.

Singida Black Stars licha ya maboresho ya kikosi chao, lakini mechi mbili zilizopita tangu kurejea kwa ligi imeshindwa kupata pointi tatu ikianza na sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Kagera kabla ya kufungwa 2-0 ugenini na KMC. Baada ya mechi mbili mfululizo Yanga kucheza Dar, Februari 23 itakwenda Kigoma kukabiliana na Mashujaa ambayo msimu huu katika mechi tisa za nyumbani imeshinda tatu, sare nne na kupoteza mbili dhidi ya Simba na Singida Black Stars. Kumbuka duru la kwanza, Yanga waliichapa Mashujaa 3-2.

Februari 28, 2025 Yanga itakuwa Mwanza kukabiliana na Pamba Jiji inayofundishwa na Kocha Fred Felix Minziro ambaye duru la kwanza wakati kikosi hicho kikipokea kichapo cha mabao 4-0 hakuwepo, timu ilikuwa ikifundishwa na Goran Kopunovic. Minziro na Pamba Jiji  aliyoiboresha dirisha dogo la usajili imeonekana kuanza kufanya vizuri ikishinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Dodoma Jiji na Azam.

MAKOCHA WANASEMAJE?

Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema katika safari ya kuufukuzia ubingwa, anaona ni bora kuwa nafasi ya pili kuliko juu.

“Ni vizuri kubaki nafasi ya pili ukiwa unaifukuzia nafasi ya kwanza kuliko kuwa wa kwanza kwani unakuwa kwenye wakati mgumu sana,” alisema hamdi huku kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema: “Ukifikiria kwamba mechi dhidi ya Yanga inaweza kuamua ubingwa, naweza kusema hapana, kila mechi inaamua jambo.”