Ukimposti mtu mwenye ‘birthday’ bila ruhusu yake faini Sh100 milioni 

Morogoro. Mabadiliko na maendeleo ya teknolojia yamekuja na faida na hasara zake katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Hilo limezilazimu mamlaka nazo kuhakikisha zinakwenda na wakati ili kudhibiti baadhi ya matokeo ya ukuaji huo wa teknolojia katika kulinda ama kupunguza athari zake kwa jamii.

Itakumbukwa kuwa miaka ya sasa linaonekana ni jambo la kawaida kwa watu kutumia mitandao ya kijamii kuposti picha ama video za ndugu, jamaa na marafiki na kuwatakia heri ya siku zao za kuzaliwa (birthday). Katika muendelezo wa mazoea hayo, wengi huchukua uamuzi wa kuposti bila kuomba ridhaa ya mhusika, ambaye pia hukutana na chapisho hilo bila kutarajia.

Hata hivyo, kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sheria namba 11 ya mwaka 2022 ya ulinzi wa taarifa binafsi huku adhabu yake iwapo shauri hilo litafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ni faini hadi ya Sh100 milioni ama jela.

Mkurugenzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Stephen Wangwe amesema sheria hiyo inazuia kwa namna yoyote ile kutangaza ama kutoa taarifa ya tarehe ya kuzaliwa ya mtu bila idhini yake.

“Ikitokea mtu ‘kamuwish’ (kumtakia heri) siku ya kuzaliwa rafiki yake kwenye mitandao ya kijamii na kama amefanya hivyo, kwa kuona tarehe ya kuzaliwa kupitia kwenye faili lake la ajira, ama mahala popote bila ya ridhaa ya mhusika basi atakuwa kwenye hatia.

“Mtendewa atakapokuja kulalamika kwetu (PDPC) tutafanya uchunguzi ikiwemo kumuhoji aliyetangaza siku ya kuzaliwa ya mwenzake akisema amepata tarehe ya kuzaliwa nje ya mhusika tutachukua hatua kwa mujibu wa kifungu cha 47 hadi 58 cha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi,” amesema Wangwe.

Amesema baadaye ya hatua hiyo ya awali, PDPC itapeleka shauri hilo mahakamani ambako kwa mujibu wa sheria mhusika akitiwa hatiani adhabu yake ni fidia isiyozidi Sh100 milioni au kifungo kulingana na mahakama itakavyopendezwa.

Wangwe amesema kama itabainika kuwa taarifa za tarehe ya kuzaliwa zimetolewa kwenye faili la kazi, mwajiri ama ofisa rasilimali watu (HR), atakuwa ni miongoni mwa washitakiwa.

Amesema mbali na makundi hayo, kumekuwepo na baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa ikiingia kwenye kutenda kosa hasa inapoweka ujumbe na kueleza siku za kuzaliwa za watu waliojiunga kwenye mtandao huo bila ridhaa ya mhusika.

” Na hii huwa inatokea hasa pale mtumiaji wa mtandao anapoandika tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa wakati akijiunga na mtandao huo, hivyo pamoja na kuwepo kwa sheria, bado watumiaji wanatakiwa kuwa makini wakati wa kujiunga kwenye mitandao mbalimbali ili kuhakikisha wanatunza usalama wa taarifa zao za binafsi.

Hata hivyo, uwepo wa sheria hiyo umeonekana kitu kipya kwa baadhi ya wananchi wakieleza kwamba, hawakuwa wakifahamu japo wamekuwa wakiwatakia heri ndugu na jamaa kwenye mitandao bila kuomba ridhaa.

Mkazi wa Nanenane mjini Morogoro, Remy Yasinti amesema hakuwahi kufahamu kuwepo kwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, lakini kwa sasa ameanza kutambua haki zake na kwamba, ni sheria nzuri yenye lengo la kulinda faragha za watu.

“Sio kila mtu anataka aweke wazi umri wake, sasa unakuta anatokea mtu mmoja anaingia kwenye akaunti yako anachukua picha na kutuma kwenye mitandao mingine na ‘kukuwish’ birthday bila ridhaa yako, kiukweli kuna wakati inakera hasa ukizingatia umri wa mtu ni siri,” amesema Yasinti.

 Ameongeza kuwa: “Unaweza kukuta mitandao mfano fulani inatoa taarifa ya ‘happy birthday’ ya mtu fulani aliyeko kwenye mtandao huo bila ridhaa yake, utaona inaandika leo ni ‘birthday’ ya fulani hii kiukweli sio sawa.

“Niliweka tarehe yangu ya kuzaliwa wakati wa kufungua akaunti, hii ilipaswa kuwa taarifa ya siri baina yangu na huo mtandao, lakini kitendo cha kutangaza kuwa leo ni ‘birthday’ yangu ni kunikosea sana, kama kweli hii sheria ipo basi isimamiwe.

Naye Shani Shariff amesema pamoja na kuwekwa kwa sheria hiyo, lakini kwake haoni kama kuna shida mtu kumposti rafiki, ndugu ama mtu anayemfahamu kama ana uhakika wa tarehe, mwezi na na mwaka wa kuzaliwa wa mhusika.

“Kitu ambacho naona kinaweza kuwa kosa ni pale ambapo mtu anakwenda kuposti tarehe ya uongo au kupekua faili la anayetaka kumpost kwa lengo la kujua tarehe, hapo ndio utasema katoa taarifa za siri,” amesema Shariff

 Ameleeza kuna wakati mwingine huyo anayelalamika kuwa tarehe yake ya kuzaliwa imetangazwa bila ridhaa yake utakuta kila mwaka anajiposti na ‘kujiwishi’ sasa katika mazingira hayo mtu ‘akimpost’ itakuwa shida?”