‘Ukiibiwa kitu chako na kikapatikana, usitoe fedha kwa polisi’

Dodoma. Wananchi walioibiwa vitu vyao na kutoa taarifa polisi wametakiwa kutotoa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kufuatilia vitu hivyo pindi vinapopatikana kwa kuwa jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa  Aprili 11, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao chake na mafundi simu na wauzaji wa vifaa vya kieletroniki vilivyotumika jijini Dodoma.

Kamanda Katabazi amesema Jeshi la Polisi lina mtandao mkubwa nchi nzima, hivyo hata kama simu iliibiwa Dodoma na ikapatikana mkoani Mwanza, jeshi hilo lina uwezo wa kuirejesha bila mhusika kulipia pesa.

Amesema kuna baadhi ya askari polisi wanaofanya kazi kwenye kitengo cha uhalifu wa mtandao ambao siyo waaminifu kwani huwadai fedha wananchi waliobiwa vifaa vyao kwa ajili ya kufuatilia vitu hivyo pindi vinapopatikana.

“Kama umeshatoa taarifa polisi kuhusu kuibiwa au kupotelewa na simu, jukumu la kuitafuta ni la Polisi, msikubali kutoa fedha ya aina yoyote ile kufuatilia kifaa chako kilichopotea kwa sababu ni jukumu letu,” amesema Katabazi na kuongeza kuwa:

Baadhi ya mafundi simu na wauzaji wa vifaa vya kieletroniki vilivyotumika wakiwa kwenye kikao na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, George Katabazi (hayupo pichani) kilichohusu kuzuia wimbi la wizi wa simu mkoani humo. Picha na Rachel Chibwete

“Hata kama simu imeibiwa Dodoma ikapatikana Mwanza mwananchi haruhusiwi kutoa fedha kwa ajili ya kufuatilia, Jeshi la Polisi lina mtandao mkubwa nchi nzima, hivyo simu hiyo itarudishwa bila kutoa fedha.”

Mbali na hilo amewatahadharisha wananchi kutokununua vitu vya wizi kwani gharama yake ni kubwa pindi itakapojulikana kuwa vitu hivyo viliibiwa kwa wizi wa kutumia silaha au hata kusababisha mauaji wakati wa wizi huo.

Amewataka wananchi kujiridhisha kabla ya kununua kitu kutoka kwa mtu (hasa vilivyotumika) kwa kutumia wenyeviti wa serikali za mitaa watendaji wa kata na maofisa polisi kata ili kujiridhisha kuwa kitu anachonunua hakijatokana na wizi.

“Na kitu cha wizi kinajulikana kwa sababu kitu kinauzwa bei kubwa dukani, mfano Sh3 milioni, lakini anakuuzia kwa Sh50,000 ni lazima ushtuke kuwa kitu hiki ni cha wizi kwani muuzaji hajui thamani ya kitu chenyewe anachokiuza,” amesema Katabazi.

Aidha, amewataka mafundi simu, kompyuta mpakato, luninga na vitu vingine vya kieletroniki hasa vilivyotumika, kujiepusha kununua vitu vya wizi kwani vinaweza kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.

Amewataka mafundi hao kutoa taarifa polisi pindi wanapopokea vifaa wanavyohisi ni vya wizi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita Jeshi la Polisi limeripotiwa simu zaidi ya 100 kuibiwa kwenye matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo wizi wa kuvunja nyumba za watu na kuiba vitu vilivyomo ikiwemo simu za mkononi.

Kwa upande wake, kiongozi wa mafundi simu Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Goliama amesema kikao hicho kilikuwa na manufaa kwao kwani wengi wa mafundi walikuwa hawajui kama kununua simu za wizi ni kosa kisheria.

Amesema mafundi wengi wamekuwa wakiingia kwenye matatizo bila kujua kwa kununua simu zilizotumika bila kujua kama ni za wizi.

“Katika kikao hiki tumejua kuwa asilimia 95 ya mafundi simu hawana nia ovu japo wapo ambao siyo waadilifu kama ilivyo kwenye kada nyingine za taaluma,” amesema Goliama.

Pia, amelalamikia baadhi ya askari polisi ambao siyo waadilifu wanaodhani kila simu ambayo wanaiflashi ni ya wizi na kusahau kuwa kuflashi simu siyo kosa kisheria bali kubadilisha muundo wake ndiyo kosa na hivyo kusababisha mafundi wengi waonekane wezi na wakati hawana kosa kisheria.

Naye, Amina Abduel amesema ni vigumu kumtambua mteja kuwa ana simu ya wizi mpaka pale itakapojulikana kuwa hajui neno siri (password) ya simu husika au neno (FRP) linaoonyesha kuwa muhusika ameingiza nenosiri lisilo sahihi kwa muda mrefu, hivyo simu imefungiwa.

Amesema mtu mwenye kifaa cha wizi akitajiwa bei kubwa ya kuflashi simu yake hukataa na kuondoka tofauti na mwenye simu ambaye ni lazima ataitengeneza simu yake ili aendelee na matumizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *