
Dar es Salaam. Wapigadebe ni sehemu ya maisha ya usafiri wa umma hasa katika maeneo ya mijini, wakijikita kutangaza au kushawishi watu kuingia kwenye daladala au magari ya abiria.
Wapo wanaotumia maneno ya kushawishi, mara nyingine kwa mbwembwe au ucheshi ilimradi gari lijae haraka na wao kupata chochote.
Katika miaka ya 1980 na 1990, sekta binafsi ya usafiri iliposhika kasi katika biashara ya usafirishaji ndipo walipoibuka wapigadebe.
Kazi hii ingawa si ajira rasmi, hakuna mikataba na wala sheria kuihusu, imekuwa chanzo cha mapato kwa wanaoifanya, baadhi wakilalamikiwa kwa kufanya fujo, lugha chafu na hata wizi.
Kadri siku zinavyosonga hata majina yanabadilika. Wapigadebe sasa wanaitwa ‘masalange’ baadhi wakitengeneza umoja na kujijengea himaya zao.
Katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam, Stanley Mwaifuga akizungumza na Mwananchi anasema wapo masalange wanaopokea abiria kwenye basi, wanalipwa posho kulingana na aliyempeleka alivyolipa nauli.
Akiwa mmoja wa masalange wanaojitafutia riziki kwa kazi hiyo isiyo rasmi, anasema wapo wanaojiita matembo wanaosubiri wengine wakiwashawishi abiria kutoka kituo cha daladala cha Mbezi Luis, wanapokaribia Kituo cha Magufuli wao huwadaka.
“Matembo hawa wana nguvu na huzitumia kufanya chochote watakacho bila kuogopa lolote,” anasema Mwaifuga.
Hata hivyo, kamanda mkuu wa ulinzi shirikishi katika Kituo cha Magufuli, Ramadhan Gape anasema matembo walikuwapo kabla ya oparesheni tokomeza wapigadebe kufanyika.
“Ulikuwa ni mchakato wa kijasiri na ulioleta tija, hawa matembo walikuwa kama walijitengenezea utawala wao hapa stendi, hawakuogopa chochote,” anasema.
Kitengo chao cha ulinzi shirikishi anasema kilipewa jukumu la kusimamia sheria, kanuni na utaratibu wa kituo ili kudhibiti wapigadebe waliosumbua abiria, wakifanya kazi chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.
Gape anasema kituo hicho kilipofunguliwa mwaka 2021 kundi la watu wasiopungua 80 walianza kupigadebe.
“Kwa miaka minne, wingi wa wapigadebe ulileta shida. Wapo waliokuwa mama lishe, waendesha bodaboda na hata makuli waliachana na kazi zao na kuanza kupiga debe,” anasema.
Anasema si wote waliofanya kazi hiyo, bali walikuwapo wenye nia ovu ya kuibia abiria.
“Abiria wengi waliibiwa mizigo, simu, kompyuta na pesa, hali hii ilisababisha kelele na kusababisha stendi ionekane haina uadilifu.
“Ukiacha ndani ya stendi, eneo la nje lilikuwa na hekaheka kuanzia kwenye mzunguko ambako kuna geti la kutokea mabasi hadi kwenye kivuko cha waenda kwa miguu, wapigadebe walitanda na kuwabughudhi abiria,” anasema.
Gape anasema eneo la kituo lilikuwa na mlundikano wa wapigadebe baadhi wakidandia bajaji, daladala na kung’ang’ania abiria, huku wakivuta mabegi na wengine wakitumia mwanya huo kuiba.
Wasemavyo abiria
Wakati Gape akieleza operesheni waliyofanya mwaka jana imesaidia udhibiti wa matembo na wapigadebe kwa jumla ndani ya kituo, abiria wanasema bado wanabughudhiwa.
Jemima Baraka, aliyekuwa Kituo cha Mbezi Luis wiki iliyopita ameieleza Mwananchi kuwa masalange wawili waliokuwa wakigombea mzigo wake walisababisha uharibifu.
“Walianza kugombana wenyewe kwa wenyewe wakigombea mzigo wangu hadi wakanichania ‘shangazi kaja’ (mfuko) langu nikiwa nashuka kituo cha daladala Mbezi Luis ili nikapande basi kwenda Kigoma,” anasema.
Athuman Mgunda, anaeleza mkasa wa kuuziwa tiketi za basi ambalo halikuwapo stendi.
Kwa upande wake, Juma Manyama anasema aliuziwa tiketi nje ya stendi, alipoingia ndani ya basi alibaini nauli aliyolipa ilikuwa kubwa na haiendani na daraja husika.
“Kuanzia siku ile nikawa mkali kwa wapigadebe wanaokimbilia abiria stendi, huwa sitaki hata wanisogelee, sema ni wasumbufu kama una hasira unaweza kugombana nao,” anasema Manyama. “Ukimjibu mmoja ukaachana naye, anakuja mwingine. Wanakera na ni wasumbufu kwa abiria, kuna wengine usipomjibu anatoa lugha mbovu.”
Husna Mbegu, anasema masalange walimrubuni akalipia nauli ya kwenda Dodoma, lakini akapelekwa kwenye basi linalokwenda Kilosa.
“Mpigadebe alinidaka nje ya stendi, hawa watu ni wanjanja. Niliibiwa kwa staili hiyo ikabidi niingie gharama nyingine,” anasema.
Udhibiti unaofanyika
Gape, kiongozi wa ulinzi shirikishi anasema Novemba, 2024 baada ya kupokea kero kadhaa kutoka kwa abiria kuhusu wapigadebe walifanya operesheni.
“Malalamiko yalikuwa ni mengi, wengine wakidai kukatiwa tiketi feki, wengine kukosa basi wakati tayari wamelipa, wengine kupewa tiketi ambazo si za kielektroniki na kero nyingine nyingi.
“Kwenye tiketi tulidili na ofisi ambayo imehusika, bila kujali aliyemwandikia tiketi abiria ni nani? tulichukua hatua na abiria alipata stahiki yake,” anasema.
Anasema baada ya operesheni hiyo, changamoto imepungua, huku wakiendelea kuwadhibiti wanaoendelea kuwabughudhi abiria kuanzia kituo cha daladala Mbezi Luis hadi stendi ya Magufuli.
“Abiria anapotoka nyumbani kuja stendi anafahamu basi gani anakwenda kupanda,” anasema.
Kamanda wa nidhamu wa ulinzi shirikishi kwenye stendi hiyo, Karama Nyilawila anasema usumbufu kwa abiria ndani ya stendi umepungua.
“Vurugu za wapigadebe zimedhibitiwa, ile hali ya watu kukimbiza vyombo vya usafiri vilivyokuwa vikileta abiria stendi haipo,” anasema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi anasema jeshi hilo limekuwa likiwadhibiti wapigadebe mara kwa mara.
“Gari la polisi likipita hapo Magufuli Terminal likikuta watu wanavunja sheria, watafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Ninachoweza kukiri hapo palikuwa na kero ya wapigadebe. Tunaendelea na oparesheni, polisi wakipitia wanakimbia, wakiondoka wanarudi, lakini tunaendelea kufanya doria mara zote,” anasema.
Akizungumzia kuhusu walinzi shirikishi anasema kundi hilo ni kama ambavyo raia mwingine wa Tanzania kwa mujibu wa sheria akiona kosa linatendeka mbele yake anaweza kukukamata.
“Akishakukamata atakupeleka polisi kwa kuvunja sheria, tunao wanafanya kazi usiku na mchana,” anasema