
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa bajeti ya mwaka 2025/2026 ukiendelea, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imebainika kukabiliwa na ukata wa kifedha, gazeti dada la The Citizen limeeleza.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya nchi wanachama kuchelewesha au kutotekeleza kabisa wajibu wao wa kuchangia bajeti ya kila mwaka, kwa mujibu wa nyaraka zilizoonwa na The Citizen.
Licha ya kuongezeka kwa idadi ya wanachama kutoka watatu hadi wanane tangu kufufuliwa kwake mwaka 2000, EAC imekuwa ikihangaika kutimiza majukumu yake ya kifedha kutokana na kutokuwa na uthabiti katika malipo kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, EAC iliidhinisha bajeti ya dola milioni 112.9 (Sh303.02 bilioni), ambapo kila nchi mwanachama ilitarajiwa kuchangia dola milioni 7 (Sh18.9 bilioni).
Hadi kufikia Aprili 25, 2025, ni Tanzania, Kenya na Uganda pekee ndiyo zilizotimiza kikamilifu ahadi zao huku Uganda ikizidisha kwa asilimia mbili kwa kuchangia dola milioni 7.16 (Sh19,3 bilioni).
Somalia, ambayo ni mwanachama mpya, imeshatoa dola milioni 3.5 (Sh9.46 bilioni), sawa na asilimia 50 ya mchango wake unaotarajiwa.
Hali ni mbaya zaidi kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini ambazo zimelipa dola 1 milioni sawa na Sh2.7 bilioni (asilimia 14) na dola 500,000 sawa na Sh1.35 bilioni (asilimia 7), mtawalia.
Burundi imetoa dola milioni 1.3 (Sh2.7 bilioni) pekee sawa na asilimia 19 ya mchango wake.
Inaelezwa kuwa licha ya malipo ya mwaka huu yanaweza kuongezeka, changamoto ya madeni ya nyuma inaendelea kuathiri kwa sababu mpaka sasa, Kenya pekee ndiyo imeweza kulipa madeni yake yote ya nyuma.
Tanzania imefanya vizuri kiasi, ikiwa na deni la nyuma la dola 122,694 (sawa na Sh331.5 milioni) pekee.
DRC inaongoza kwa deni kubwa zaidi la nyuma la dola milioni 20.7 (Sh55.9 bilioni).
Inafuatiwa na Burundi yenye deni la dola milioni 15.8 (Sh42.7 bilioni) na Sudan Kusini inayodaiwa dola milioni 15.1 (Sh40.5 bilioni).
Somalia na Rwanda wana deni la dola milioni 3.5 (Sh9.46 bilioni) na milioni 1.8 (Sh4.86 bilioni), mtawalia.
Kwa mujibu wa ripoti za ndani na za wachambuzi wa kikanda, hali ya kutokuwepo kwa usawa katika mchango wa fedha imevuruga shughuli muhimu, kuchelewesha miradi na kuibua maswali kuhusu uendelevu wa programu za EAC.
“Mkutano wa kushinikiza nchi zinazoshindwa kuchangia unaendelea ili kuzisihi kutekeleza wajibu wao wa kifedha,” amesema Ofisa mwandamizi wa EAC anayehusika na mijadala ya bajeti.
Tangu zamani, ukosefu wa fedha umekuwa ukidhoofisha shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya kuvuka mipaka, operesheni za amani na usalama na ulinganifu wa sera za biashara na forodha.
Ofisa huyo amesema licha ya kuongezeka kwa nchi wanachama, matatizo ya fedha ya EAC yamezidi kuwa makubwa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa bajeti ya sasa imelenga kufadhili programu za kimkakati kama Mfumo wa Forodha wa Pamoja (SCT), maandalizi ya sarafu ya pamoja ya EAC pamoja na juhudi za kuimarisha amani, utawala bora na muunganiko wa masoko ya kikanda.
“Uaminifu wa EAC unazidi kudorora, hasa pale nchi wanachama zinaposhindwa kutekeleza makubaliano waliyoyapitisha wao wenyewe,” amesema Amon Kimei, mchambuzi wa masuala ya muungano wa kikanda.
Kimei amesema huwezi kuwa na muungano wa wa nchi wenye nguvu wakati hata shughuli za msingi haziwezi kufadhiliwa.
“Sasa ukosefu huu wa fedha si tu unachelewesha utekelezaji wa miradi, bali pia unaathiri ustawi wa wafanyakazi, shughuli za kiutawala na ushirikiano wa kidiplomasia na mashirika ya maendeleo ya kimataifa,” amesema Kimei.
Ili kukabiliana na hali hii ya kifedha, EAC kwa miaka kadhaa ilipendekeza mbinu mbadala za ufadhili ikiwa ni pamoja na ushuru wa asilimia 0.2 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya jumuiya sawa na ule wa Umoja wa Afrika.
Hata hivyo, pendekezo hilo limekumbwa na upinzani wa kisiasa na halijatekelezwa.
Njia nyingine inayoendelea kujadiliwa ni ya kubadilisha mfumo wa kuchangia, ili kuruhusu nchi zenye uchumi imara zaidi kuchangia zaidi, na kupunguza mzigo kwa nchi changa au zenye uchumi dhaifu.
Lakini hadi mwaka 2025, pendekezo hilo nalo bado limekwama.
“Tatizo si ukosefu wa mawazo ni ukosefu wa nia ya kisiasa,” amesema James Manyika, mchumi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mnyika amesema hakuna nchi inayotaka ionekane kama inaisaidia nyingine, bali ni mpaka pale mtazamo huo utakapobadilika.
Ili kulinda mustakabali wa jumuiya hiyo, wataalamu na maofisa wanazitaka nchi wanachama kulipa madeni yao haraka.
“Ukosefu wa fedha si tu unakwamisha shughuli, bali pia unadhoofisha imani na mshikamano ulioasisi jumuiya hii,” amesema John Silayo, mwanadiplomasia na mchambuzi wa kisiasa.
Hata hivyo, amesisitiza haja ya kuwa na mfumo wa kifedha unaozingatia uwezo wa kiuchumi wa kila mwanachama.
“Ingawa michango sawa inaweza kuonekana kuwa ya haki kwa mtazamo wa karatasi, haizingatii tofauti za kiuchumi,” amesema.