
Musoma. Uwanja wa ndege wa Musoma unaokarabatiwa na kujengwa gharama ya zaidi ya Sh35 bilioni sasa unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu baada ya ujenzi huo kushindwa kukamilika kwa miaka mitatu, kutokana na changamoto mbalimbali ikiwepo ukosefu wa fedha.
Awali uwanja huo ulioanza kukarabatiwa na kujengwa Aprili 2021 ulitarajiwa kukamilika Desemba 2022.
Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Beijing China Construction Engineering Group (BCEG) ilielezwa kuwa amekuwa akitekeleza mradi huo kwa kusuasua kutokana na kuchelewa kwa malipo kutoka serikalini, ambapo alikuwa akidai zaidi ya ShSh3 bilioni kwa mujibu wa taratibu kutokana na kazi aliyokwishaifanya.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ,Evans Mtambi aliyefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo leo Aprili 13,2025, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh8.2 bilioni ili kuendelea ujenzi wa uwanja huo kwa kasi na kukamilika kwa muda uliopangwa.
“Tayari mkandarasi ameelekezwa kuongeza nguvu kazi ikiwa ni pamoja na vifaa na muda wa kufanya kazi utekelezaji wa maagizo hayo umeanza, ambapo umefika asilimia 58 tunatarajia ukamilike Septemba mwaka huu. Mbali na hizi Sh8.2 bilioni zilizolipwa awamu hii pia awali Serikali ilikwishalipa zaidi ya Sh10 bilioni kama malipo ya awali,” amesema Maribe.
Kuhusu fidia, Maribe amesema tayari wananchi wote waliotakiwa kulipwa wamelipwa na wamepisha ili mradi uweze kutekelezwa, ambapo zaidi ya Sh8 bilioni zimelipwa kama fidia kwa wamiliki wa nyumba zaidi ya 100 zilizofanyiwa tathmini ili kupisha mradi huo.
Amesema uwanja huo unatarajiwa kuongezwa urefu na kufika kilomita 1.75 kutoka kilomita 1.6 za sasa na kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo pamoja na mambo mengine ujenzi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, njia ya maungio, jengo la zimamoto na gari la zimamoto pamoja na uzio.
Kwa upande wake Meneja wa uwanja huo, Frank Msofe amesema tayari zaidi ya Sh5.2 bilioni zimeidhinishwa na mthamini mkuu wa Serikali kwa ajili ya malipo ya fidia kwa kaya 58 zilizopo jirani na uwanja huo, ili kupisha eneo la ujenzi wa jengo la abiria ambalo awali halikuwa kwenye mradi.
Amesema kabla ya ujenzi wa jengo hilo wana mpango wa kuboresha miundombinu iliyopo ili iweze kutumika baada ya ukarabati unaoendelea kukamilika.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi huo, Mtambi amewaagiza wasimamizi wa miradi mkoani humo kuhakikisha yote inakamilika kwa wakati bila kuwepo kwa kisingizio cha aina yoyote.
“Hapa taarifa yenu na hali halisi ya utekelezaji wa mradi huu inaonyesha kuwa mtakamilisha hata kabla ya Septemba, nitumie fursa hii kuwaagiza wasimamizi wengine wa miradi kuiga mfano huu wa Tanroads sitaki kusikia tuko kwenye mchakato nataka kuambiwa tumefanya kile, tunafanya hiki,” amesema
Mtambi amesema Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi mbalimbali iliyokuwa ikisuasua hivyo ni matarajio yake kuwa itakamilika kwa muda uliopangwa.
Kuhusu uwanja huo, Mtambi amesema Mkoa wa Mara unautegemea uwanja huo kama sehemu mojawapo ya kimkakati kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha uchumi kupitia sekta mbalimbali zikiwamo za utalii na biashara.
“Uwanja huu utakapokamilika utasaidia sana katika kuinua uchumi wa mtu mmojammoja na mkoa kwa ujumla, kwani kwa kutumia fursa za rasilimali tulizonazo kama madini, ziwa, utalii, mifugo na mambo mengine huu uwanja utakuwa kiungo muhimu katika suala zima la usafiri na usafirishaji,”amesema Mtambi.