Ujumbe wa HAMAS wafanya ziara ya kushitukiza nchini Misri kuhusu usitishaji vita

Timu ya mazungumzo ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ikiongozwa na Khalil al Hayya imefanya ziara ya kushitukiza mjini Cairo Misri kwa ajili ya mazungumzo ya kusimamisha vita.

Hayo yametangazwa leo na mtandao wa habari wa al Arabi al Jadid na kusema kuwa, viongozi wa Misri ndio walioitaka timu hiyo ya HAMAS kuelekea Cairo kwa ajili ya usitishaji vita huko Ghaza, baada ya viongozi hao wa Misri kufanya mazungumzo ya simu na pande kadhaa kuhusu suala hilo.

Timu hiyo ya HAMAS imeonana na maafisa usalama wa Misri akiwemo mkuu mpya wa usalama wa taifa wa nchi hiyo Meja Jenerali Hassan Mahmoud Rashad na wametilia mkazo wajibu wa kukomeshwa haraka mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Ghaza.

HAMAS inahimiza kukomesha haraka jinai za Israel huko Ghaza

Hivi karibuni serikali za Misri na Marekani zilifanya mazungumzo kuhusu pendekezo la Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusiana na kupelekwa askari wa kimataifa katika eneo la Filadelfia kwenye mpaka wa Misri na Ukanda wa Ghaza kabla ya vikosi vamizi vya Israel kuondoka kwenye eneo hilo. 

Inatarajiwa kuwa karibuni hivi  timu za mazungumzo na upatanishi zitaelekea katika mji mkuu wa Qatar, Doha kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu usitishaji vita huko Ghaza, Palestina. 

Kiongozi mmoja wa HAMAS ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesisitiza kuwa, harakati hiyo iko tayari kwa ajili ya kusimamisha vita kwa sharti kwamba utawala wa Kizayuni ulazimishwe kuheshimu usitishaji vita huo, uondoe wanajeshi wake katika Ukanda wa Ghaza, uruhusu kurejea wakimbizi katika maeneo yao na baadaye kuchukuliwe hatua madhubuti za kubadilishana mateka.