Ujue udanganyifu wa ‘Ponzi’ na chimbuko lake-1

Kwenye sekta ya fedha, kuna mifumo michache ambayo huleta hofu kwa wawekezaji na watu wa kawaida. Miongoni mwa mifumo hiyo ni “mfumo wa Ponzi.”

Mfumo huo ulianza kujulikana karne ya 20 na uliitwa Ponzi kutokana na jina la Mwanzilishi ambaye aliitwa Charles Ponzi.

Ponzi alizaliwa Lugo, Italia na akajulikana mwanzoni mwa miaka ya 1920. Aliwaahidi wateja faida ya asilimia 50 ndani ya siku 45 au faida ya asilimia 100 ndani ya siku 90, kwa kununua tiketi za kujibu posta kwa bei nafuu katika nchi nyingine na kuzirejesha kwa thamani yake halisi nchini Marekani kama aina ya biashara ya kubadilishana (arbitrage).

Katika ukweli, Ponzi alikuwa akilipa wawekezaji wa awali kwa kutumia uwekezaji wa wawekezaji wa baadaye. Ingawa aina hii ya mpango wa udanganyifu wa uwekezaji haikuanzishwa na Ponzi, ilijulikana sana na yeye kiasi kwamba sasa inaitwa “mpango wa Ponzi.” Mpango wake ulifanyika kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuanguka, na kuwagharimu “wawekezaji” wake dola milioni 20.

Mfumo ya Ponzi umeendelea kuwa mojawapo ya utapeli mkubwa wa kifedha kwa miongo mingi. Huu ni aina ya udanganyifu unaotoa matumaini ya watu kupata fedha kwa haraka na kirahisi, lakini ukweli wa kusikitisha ni kwamba huacha wawekezaji wakiwa na mikono mitupu na imani yao kuvunjika.

Mfumo wa ponzi ni Nini?

Mfumo wa Ponzi ni aina ya udanganyifu wa uwekezaji unaoahidi faida kubwa kwa hatari kidogo au hakuna kabisa. Mfumo huu unafanya kazi kwa kuchukua fedha kutoka kwa wawekezaji wapya na kuzitumia kulipa faida kwa wawekezaji wa awali. Mwanzilishi wa Ponzi hafanyi uwekezaji katika biashara yoyote halali au mali, badala yake hutegemea mtiririko wa fedha kutoka kwa wawekezaji wapya kudumisha mzunguko wa fedha.

Ili mfumo wa Ponzi uweze kudumu wawekezaji wapya wanatakiwa kujiunga na ikiwa mtiririko wa uwekezaji mpya utasimama au kupungua, muundo mzima utafeli, na wawekezaji waliobaki wataweza kupoteza fedha zao. Kwa kifupi, mifumo ya Ponzi inategemea “kumwibia Peter ili kumlipa Paul.”

Kwa bahati mbaya, mifumo ya Ponzi siyo ya kihistoria pekee. Kwa miaka mingi, udanganyifu maarufu kadhaa zimefuata mfano wa Ponzi. Kwa Udanganyifu maarufu nchini tanzania ni kama kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), Kampuni ya TELEXFREE iliyokuwa inafanya biashara ya upatu Afrika mashariki mwaka 2014, Kampuni ya Best way Capial Management (BCM) iliyosajiliwa mwaka 2019, Kampuni ya Kalynda E-Commerce Limited inayojishughulisha na biashara mtandao iliyosajiliwa Mwaka 2022 na nyingine nyingi zinazoendelea kuchepuka kila siku.
Itaendelea wiki ijayo.