Ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato wafikia asilimia 85

Dodoma. Ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 85 kwa njia za kurukia ndege, huku majengo ya abiria yakifikia asilimia 51.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Augustino Vuma ameyasema hayo leo Jumatano, Machi 12, 2025 baada ya kamati yake kutembelea uwanja huo.

Vuma amesema mradi huo ni wa kimkakati wa kujenga majengo ya abiria yatakayogharimu Sh190 bilioni na njia ya kurukia ndege itakayogharimu Sh160 bilioni.

“Kamati tumeshuhudia maana kuona ni kuamini, karatasi pekee hazitoshi, kazi kubwa inaendelea na makubwa yamefanyika ukikamilika kwa wakati utasaidia Watanzania wanaousubiri kwa hamu kubwa,”amesema Vuma.

Vuma amesema mradi huo una ubora na mkandarasi yupo ndani ya muda na kukamilika kwake kutasisimua uchumi wa Mkoa wa Dodoma kwa sababu ndege kubwa zitatua na kupaa.

Amepongeza Wizara ya Uchukuzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ambao ni watekelezaji wakuu wa mradi huo. “Tunataka ukamilike kwa wakati.”

 Awali akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu Tanroads, Mohamed Besta amesema utekelezaji unakwenda vizuri na watafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na kamati.

Kwa mujibu wa Tanroads, awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanja hicho itakuwa na uwezo wa kuhudumia Boeing 787-8 (Dreamliner) ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 350.

Februari 2020 Serikali na Benki ya Afrika (AfDB), walitiliana saini mkataba wa mkopo kwa ajili ya ujenzi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 329.29 milioni.

Ujenzi wa njia za kurukia ndege unatarajiwa kukamilika Aprili 2025, huku sehemu ya pili ya mradi huo inayohusisha majengo ya abiria ikikamilika Julai 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *