Arusha. Kufuatia tukio la Aprili 25, 2023 lililosababisha vifo vya watu wanne wa familia moja baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko katika eneo la King’ori, wilayani Arumeru, Serikali imeanza ujenzi wa madaraja mapya kama hatua ya kudumu ya kukabiliana na maafa na changamoto za miundombinu.
Madaraja hayo mawili, yanayojengwa katika eneo hilo ambalo lipo kwenye barabara kuu ya Arusha-Moshi, yanatajwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa kero ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo, hasa wakati wa mvua kubwa.
Eneo hilo mara kwa mara hujaa maji kiasi cha barabara kufungwa kwa muda, hali inayosababisha usumbufu kwa wasafiri na kuathiri shughuli za uchumi.

Mwonekano wa ujenzi wa daraja katika eneo la King’ori wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, leo Mei 20, 2025 ambapo ujenzi wake unaendelea kufuatia eneo hilo kuwa korofi na kusababisha maji kujaa katika barabara kuu ya Arusha- Moshi wakati wa mvua.
Akizungumza leo Jumanne, Mei 20, 2025 wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema Serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha maisha ya wananchi hayapotei tena kutokana na changamoto za miundombinu isiyo imara.
“Katika barabara hii mwaka 2023 watu walipoteza maisha kutokana na mafuriko. Serikali haiwezi kuruhusu hali kama hii ijirudie. Haya madaraja ni sehemu ya mkakati wa kulinda maisha ya Watanzania na kurahisisha shughuli za kiuchumi,” amesema Makonda.
Ameongeza kuwa barabara hiyo ni kiunganishi muhimu kati ya mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, na pia inahudumia wageni kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), hivyo uwekezaji katika miundombinu hiyo ni wa kimkakati kwa maendeleo ya uchumi wa kitaifa na kikanda.

Makonda amesema mbali na King’ori, madaraja mengine yanajengwa katika maeneo ya Kisongo na Longido.
“Yote haya ni kuhakikisha kuwa hata wakati wa mvua kubwa, shughuli za usafirishaji hazisimami. Hii ni hatua muhimu kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utalii, biashara na usafirishaji wa bidhaa,” ameongeza Makonda.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amesema Serikali kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia imepokea Sh11.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo matatu.
Amesema kati ya fedha hizo, Sh4.6 bilioni zitatumika kukamilisha madaraja mawili ya King’ori, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa Massawe katika eneo la Tanganyet, wilayani Longido, Tanroads inajenga daraja la mita 40 litakalogharimu Sh4.7 bilioni.
Ujenzi huo umesuasua kutokana na mvua kubwa, lakini unatarajiwa kuanza rasmi ndani ya wiki moja na kukamilika Januari 2026.
Hii ni baada ya kingo za daraja hilo kubomoka Novemba 2023, jambo lililozua hofu kuhusu uwezekano wa kukatika kwa mawasiliano kati ya Tanzania na Kenya.
Kwa upande wa Kisongo, daraja linalojengwa limegharimu Sh2.6 bilioni na limekamilika, sasa liko katika hatua ya kuwekewa tabaka la lami.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha hizi. Zitaondoa kero kubwa iliyokuwepo hasa kipindi cha mvua ambapo barabara ya King’ori ilikuwa inafungwa kwa zaidi ya saa nne kutokana na mafuriko,” amesema Mhandisi Massawe.
Ameongeza kuwa kuna mpango wa upanuzi wa barabara kuu ya Arusha–Moshi kuwa njia nne kutoka Tengeru hadi KIA, ambapo usanifu wake uko katika hatua za mwisho na mzabuni anatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.

Pia, imeelezwa hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha miundombinu kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Julius Loota, dereva wa magari ya mizigo, amesema: “Hili ni jambo la kupongezwa. Tumekuwa tukikwama kwa saa nyingi kipindi cha mvua. Ujenzi wa madaraja haya utarahisisha sana kazi zetu.”